Nelson Mandela Asherehekea Miaka 95 yu-Mahututi

Wananchi wa Afrika Kusini wakiwa wameleta maua na jumbe za pongezi kumpongeza Nelson Mandela kutumiza miaka 95 na kumtakia afya njema.

Wananchi wa Afrika Kusini wakiwa wameleta maua na jumbe za pongezi kumpongeza Nelson Mandela kutumiza miaka 95 na kumtakia afya njema.

RAIS wa zamani wa nchi ya Afrika Kusini, mzee Nelson Mandela Julai 18, 2013 ametimiza miaka 95 huku akiwa bado mgonjwa na amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU). Kiongozi huyo maarufu Afrika na duniani kote kwa muda wa wiki takribani sita sasa amelazwa akisumbuliwa na mapafu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya nchi hiyo ilisema hali ya mkongwe huyo inaonesha kuimarika kidogo licha ya kwamba bado yupo ICU. Salamu zimemiminika kumpongeza mzee Nelson Mandela na kumtakia nafuu ya haraka.

Rais Barack Obama wa Marekani amesema katika salamu zake kwamba yeye na familia yake walitiwa hamasa na ushujaa wa Mandela, baada ya kutembelea gereza alikofungiwa kwa miaka mingi wakati wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi. Mapema leo Ikulu ya Afrika Kusini imetoa tangazo linaloarifu juu ya afya ya mzee Mandela.

“Madiba anabakia hospitalini mjini Pretoria, lakini madaktari wanaomtibu wanathibitisha kuwa hali yake inaboreka taratibu”, lilisema tangazo hilo, likitumia jina la kiukoo la Mandela..Madiba.

Mbali na kumpongeza Mandela kwa kutimiza miaka 95, Rais Obama ametoa wito kwa watu kuadhimisha siku ya Mandela wafanya kazi za kujitolea kwa kuenzi jina lake. Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amewataka watu kuiga mchango wa Mandela na kujitolea kwake, kwa kuongeza juhudi za kuiendeleza jamii yao. Zuma mwenyewe atawakilisha mtazamo wa Mandela wa kuzileta pamoja jamii, kwa kuwapa nyumba watu masikini weupe.

Katika juhudi hizo, waendesha baskeli watafanya usafi mitaani, wafanyakazi wa kujitolea watapaka shule rangi, na wanasiasa watashiriki katika miradi mingine ya kujitolea kwa muda wa dakika 67, kutambua miaka 67 ambayo Mandela amekuwa mtumishi wa umma. Aidha, wanafunzi wataanza siku yao shuleni kwa kuimba wimbo ‘Happy Birthday Mandela’ wakimtakia heri na kumpongeza kwa kutimiza miaka 95.

Shughuli nyingine itakayofanyika kuadhimisha miaka 95 ya Nelson Mandela, ni kumkabidhi mkongwe huyo kitambulisho kipya cha kisasa, ambacho kitapokelewa kwa niaba yake na bintiye Zindzi.
Mandela anasifiwa kote duniani kwa kusimama kidete dhidi ya ubaguzi wa aina yoyote. Tukio hilo litakuwa na viashiria mbali mbali kama kumbu kumbu ya enzi za ubaguzi wa rangi, ambapo raia weusi walilazimishwa kubeba vitambulisho, na hawakuruhusiwa kutembea katika baadhi ya maeneo, kwa baadhi ya nyakati.

Mwaka 2010, Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe 18 Julai kuwa siku ya Mandela, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Nobel ya Amani, lakini mwaka huu, siku hii imekuwa na umuhimu mkubwa zaidi.
Mandela amalazwa hospitalini kwa siku 41 sasa akiugua maambukizi ya mapafu, na kwa muda mrefu hali yake imetajwa kuwa mbaya, lakini ambayo imedhibitiwa na madaktari.

Watu wa familia yake wamesema kuwa hali hiyo imeimarika kwa kiasi fulani, na anaweza kupumua kwa msaada wa mashine. Binti yake Zindzi jana aliliambia shirika la habari la Sky News kwamba kuna wakati walipokuwa wamekata tamaa wakijiweka tayari kupokea habari mbaya, na kuongeza kuwa kwa sasa anawapa matumaini. Watu mbalimbali mashuhuri na wa kawaida wameahidi kujiunga na wananchi wa Afrika Kusini, kumuunga mkono Mzee Mandela katika siku kuu yake ya kuzaliwa.

-DW