Nelson Mandela Aendelea Kupata Nafuu

RAIS wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, anayetibiwa kwa ugonjwa wa mapafu, anaendelea vyema na matibabu yake na kwamba hali yake imeimarika katika saa 24 zilizokamilika. Taarifa za kuugua kwa Mandelea zimewatia watu wasiwasi mkubwa hasa wapenzi wa mpiganiaji haki huyo.

Bwana Mandela,mwenye umri wa miaka 94, alikimbizwa katika hospitali ya kijeshi, mjini Pretoria, siku ya Jumamosi. Madaktari wanaomtibu Mandela wameelezea kuridhika na anavyopata nafuu. Hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Ofisi ya Rais Jacob Zuma.

Taarifa za bwana Mandela kuendelea kuwa hospitalini, zimezua wasiwasi nchini Afrika Kusini. Magonjwa ya mapafu yanaweza kusababishwa na virusi au viini tete. Pia yanaweza kusambazwa kupitia kwa kikohozi au kupiga chafya na yanaweza kuambukizwa kwa kugusa sehemu ambazo mgonjwa amegusa.

Kuna majina tofauti ya magonjwa ikizingatiwa sababu na sehemu ya mwili ambapo ugonjwa ule umeambukizwa.
Homa ya mapafu, husababishwa na viini tete vijulikanavyo kama (Streptococcus pneumoniae) na huathiri sehemu za kupumua kwenye mapafu. Mkamba ni ugonjwa unaoathiri njia ya kupumua na husababishwa sana na mafua au virusi vinavyosababisha mafua.

Wazee ndio huathirika zaidi na ugonjwa huu kwa sababu ya homa ya mapafu pamoja na watu walio pungukiwa na kinga ya mwili. Bwana Mandela amewahi kutibiwa kwa mara nyingine ugojwa wa kifua kikuu Bwana Mandela aliwahi kutibiwa kwa ugonjwa wa kifua kikuu ambao unaathiri mapafu.

Magonjwa mengi ya mapafu hutibiwa kwa madawa, mgonjwa kupumzika au kupata vinywaji vingi, lakini katika umri wake wa miaka 94, bwana Mandela amedhoofika na madaktari wanamkagua kwa karibu kuona atakavyoendelea na matibabu.

-BBC