TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza tarehe za Uchaguzi wa Ubunge na Udiwani katika Jimbo na Kata ambazo hazikufanya Uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Octoba 2015 kwa sababu mbalimbali. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan K. Kailima imezitaja tarehe hizo kuwa ni tarehe 15 Novemba na tarehe 13 Decemba 2015.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inawatangazia wananchi wote kuwa Uchaguzi wa Ubunge na Udiwani katika Jimbo na Kata ambazo hazikufanya Uchaguzi tarehe 25 Octoba 2015 kwa sababu mbalimbali isipokuwa kifo, Uchaguzi huu sasa utafanyika tarehe15 Novemba na tarehe 13 Decemba 2015,” ilieleza taarifa hiyo.
Jimbo na Kata zitakazo husika kufanya uchaguzi 15 Novemba 2015 ni LULINDI– MASASI DC, KILOLENI-URAMBO DC, MALAMBO-NGORONGORO DC, NGARESERO, MIZIBAZIBA-NZEGA DC, TONGI, LUDETE-GEITA, BUKULA-RORYA, BUPAMWA-KWIMBA DC, MWAMBANI-CHUNYA DC, ITEWE, MKOLA, MBUYUNI, ISEBYA-MBOGWE DC, MATONGO-BARIADI DC, MAJENGO-KOROGWE DC, SONGWE-KILINDI DC, MKONGOBAKI-LUDEWA DC, MAHANJE-MADABA DC, KAGERA-KIGOMA UJIJI, MILEPA-SUMBAWANGA, RUJEWA-MBARARI DC, MAGAMBA-MPANDA DC, MKONGO GULIONI-NAMTUMBO, LISIMONJI na SARANGA-KINONDONI.
Maeneo mengine ambayo yatafanya uchaguzi 13 Decemba 2015 ni pamoja na kata za, IPALA-DODOMA DC, NYAMILOLELWA- GEITA DC. Mkurugenzi Kailima alisema vituo vya kupigia Kura ni vile vilivyotumika wakati wa upigaji Kura za Urais Oktoba 25, 2015, huku akisisitiza kwamba vituo vitafunguliwa saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni.
Alisema wanaoruhusiwa kupiga Kura ni wale walio na kadi za Mpiga Kura na wamo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hata hivyo alisema tareheya Uchaguzi katika Jimbo la Kijitoupele Zanzibar itatajwa hapo baadaye hivyo kuwataka wapiga kura wa eneo hilo kuendelea kuwa na subra wakati utaratibu ukiandaliwa.