KUHUSU KUMALIZIKA KWA KIBALI CHA WATAZAMAJI WA UCHAGUZI MKUU WA RAIS, WABUNGE NA MADIWANI MWAKA 2015
Kwa mujibu wa Kifungu cha 63 (4) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepewa mamlaka ya kuandaa na kutoa mialiko kwa Watazamaji wa Uchaguzi wa Ndani na Nje ya Nchi.
Ili kuweza kutekeleza matakwa ya kisheria, Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliandaa Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 pamoja na Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za mwaka 2015 (Uchaguzi wa Madiwani) ambazo zilitoa maelezo kuhusu mialiko, sifa au kukosa sifa na usajili wa watazamaji wa Ndani na Nje.
Aidha, Kanuni hizo zimeainisha maelekezo kuhusu muda wa watazamaji, haki zao, mambo wasiyotakiwa kufanya, utoaji wa taarifa kwa Umma na uwasilishaji wa taarifa za Watazamaji kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015 pamoja na Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za mwaka 2015 (Uchaguzi wa Madiwani) Tume ilito Mwongozo wa Watazamaji wa Uchaguzi wa mwaka 2015 ulioelezea pamoja na mambo mengine mipaka ya kazi ya Utazamaji na ukomo wake.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia Kanuni tajwa, ilipokea maombi ya Watazamaji wa Uchaguzi na kuwapatia Vitambulisho pamoja na barua za kuwatambulisha kuwa wao ni watazamaji wa Uchaguzi wa Ndani na Nje ya Nchi. Kwa mujibu wa Vitambulisho na barua hizo, ukomo wa kazi ya Utazamaji wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ilikuwa ni tarehe 10 Novemba, 2015.
Kwa maana hiyo, hakuna Mtazamaji yoyote wa Uchaguzi wa Ndani na Nje ya Nchi anayeruhusiwa kuendelea na kazi za Utazamaji au zinazofanana na hizo baada ya tarehe 10 Novemba, 2015 bila kuomba tena Tume na kupewa Kibali iwapo Tume itaridhia ili aweze kutazama Uchaguzi katika majimbo na Kata zilizoahirisha Uchaguzi.
Taasisi yoyote inayomtuma mtu au watu kufanya zoezi la utazamaji au linalohusiana na hilo kwa kisingizio cha kuwa Mtazamaji wa Ndani au Nje ya nchi bila kupata Kibali cha Maandishi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi atakuwa 3 amekiuka Sheria za nchi na ieleweke wazi kuwa Tume haitaitetea Taasisi hiyo au mtu ambaye anafanya utazamaji wa Uchaguzi bila ya kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuhusiana na chaguzi zilizoahirishwa, Mtazamaji yeyote anayetaka kuja kutazama Uchaguzi anatakiwa kuleta maombi
upya kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Imetolewa na: Kailima Ramadhani
MKURUGENZI WA UCHAGUZI
18.11.2015