Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepokea vifaa mbalimbali vikiwemo vibanda vya kupigia kura (vituturi), masanduku ya kupigia kura, lakiri za kufungia masanduku pamoja na vifaaa vingine vitakavyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu nchini.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Ununuzina Ugavi Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Eliud Njaila alipokuwa akiongea na waadishi wa habari wakati wa kupokea vifaa hivyo leo jijini Dar es salaam.
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inapenda kuwajulisha Watanzania na wadau wote wa uchaguzi kuwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu yamekamilika na vifaa vyote muhimu vya kuendeshea zoezi hilo vimekamilika” alisema Bw. Njaila.
Akisisitiza juu ya gharama ya vifaa hivyo, Bw. Njaila alisema kuwa vifaa mbalimbali vya uchaguzi zikiwemo karatasi za kupigia kura vyote kwa ujumla vinathamani ya Sh. 41,868,045,168 bila kuweka gharama ya ununuzi wa mashine za BVR.
Aidha, Bw. Njaila alisema kuwa vituturi vinaendelea kutengenezwa hapa nchini ambapo kila siku idadi ya vituturi 8000 vitakuwa vinakabidhiwa kwa kwa tume ya uchaguzi tayari kwa kusambazwa nchi nzima katika kila halmashauri kabla ya zoezi la kupiga kura Oktoba 25 mwaka huu.
Vifaa kwa ajili ya zoezi la uchaguzi vitasambazwa kwa kanda kuanzaia kanda ya Ziwa, kanda ya kati, kanda ya kusini, kanda ya magharibi, kanda ya nyanda za juu kusini, kanda ya kaskazini, kanda ya mashariki pamoja na Zanzibar kulingana na utaratibu uliowekwa na NEC na ZEC.