*Awasili Ikulu Kupongezwa na JK
Na Joachim Mushi, Dar es Salaam
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imemtangaza aliyekuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Pombe Magufuli kuwa mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa rais uliofanyika Oktoba 25, 2015 baada ya kumalizika zoezi la kujumlisha matokeo ya kura za urais toka maeneo mbalimbali.
Akitangaza matokeo hayo, Jaji msaafu Damian Lubuva alisema amemtangaza Dk. Magufuli kuwa ndiye mshindi wa kinyang’anyiro hicho baada ya kupata jumla ya kura 8,882,935 ikiwa ni sawa na asilimia 58.46 huku mpinzania wake wa karibu Edward Ngoyai Lowassa akifuatia kwa kujipatia kura 6,072,848 ikiwa ni sawa na asilimia 39.97.
Jaji Lubuva alisema mshindi wa tatu amekuwa ni mwanamama pekee aliyeshiriki kinyang’anyiro hicho akitokea chama cha ACT, Wazalendo, Mama Anna Elisha Mghwira aliyejipatia jumla ya kura 98,763 ikiwa ni sawa na asilimia 0.65, huku nafasi ya nne ikichukuliwa na mgombea kutoka chama ADC, Chief Lutalosa Yemba aliyejipatia jumla ya kura 66,049 ikiwa ni sawa na asilimia 0.43.
Nafasi ya tano imeenda kwa mzee Hashim Rungwe Spunda wa Chama cha CHAUMMA aliyejipatia jumla ya kura 49,256 ambapo ni sawa na asilimia 0.32, huku wagombea wengine Lyimo M. Elifasio wa TLP aliyepata kura 8,028, Kasambala J. Maliki wa NRA kura 8028 na Dovutwa F. Nasoro UPDP 7785 na wote wakiwa na asilimia 0.05.
Jaji Lubuva alisema jumla ya wapigakura 23,161,440 walijiandikisha huku waliopiga kura wakiwa jumla 15,589,639 sawa na asilimia 67.31 na jumla ya kura halali zilikuwa ni 15,193862 (97.46%); idadi ya kura zilizokataliwa ilifikia 402,248 (2.58%).
Dk. Magufuli pamoja na mgombea mwenza wake, Mama Samia Suluhu Hassan watakabidhiwa hati zao za ushindi kesho ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee ikiwa ni utambulisho rasmi kama washindi tayari kuelekea hatua nyingine ya kuapishwa na kuweza kuliongoza taifa la Tanzania.
Hata hivyo tayari mpinzani wake Lowassa amepinga matokeo hayo na kugoma kutia saini akidai hayakuwa sahihi, jambo ambalo Jaji Lubuva alisema halimzuii kumtangaza mshindi wa mchakato huo. Baada ya ushindi huo sasa Dk. Magufuli ndiye mrithi wa Rais Jakaya Kikwete ambaye anapokea kijiti cha wadhifa huo.
Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete (kushoto) akimpa mkono wa pongezi Dk. John Magufuli baada ya kutangazwa kushinda urais Tanzania. |
Rais Jakaya Kikwete akimpa mkono wa pongezi Dk. John Magufuli baada ya kutangazwa kushinda urais Tanzania ikulu Dar es Salaam. |
Rais Jakaya Kikwete akimpa mkono wa pongezi Dk. John Magufuli baada ya kutangazwa kushinda urais Tanzania ikulu Dar es Salaam. Kushoto niĀ Mke wa RaisĀ Mama Salma Kikwete. |
Dk Magufuli akipokea pongezi mbalimbali kwa njia ya simu muda mfupi baada ya kutangazwa alipokuwa Ikulu kupongezwa na Rais Kikwete. |
Dk. Magufuli na Rais Kikwete katika mazungumzo ya pongezi Ikulu jijini Dar es Salaam. |