Ndesamburo, mchumba wa Dk. Slaa wakwamisha kesi

Dr. Slaa, Mh. Ndesamburo, na Mh. Mbowe walipohudhuria kesi Mahakamani siku za nyuma

Na Janeth Mushi, Arusha

KESI inayowakabili baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu wa Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho taifa Freeman Mbowe na Katibu Mkuu Dk. Wilbroad Slaa ya kufanya kusanyiko pasipo kibali imekwama tena kuanza kusikilizwa kutokana na watuhumiwa wawili kutokuwepo mahakamani hapo

Aidha kesi hiyo ambayo imekwama kuanza kusikilizwa kwa zaidi ya mara
mbili, jana ilikuwa ianze usikilizwaji wa awali katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi mkoa wa Arusha, ilikwama kutokana na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo na mchumba wa Dk. Wilbroad Slaa, Josephine Mashumbusi kutokufika mahakamani hapo tena.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Charles Magessa, Wakili wa
Upande wa Serikali Joseph Pande aliieleza mahakama hiyo kuwa jana kesi hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa (Usikilizwaji wa awali).

Upande wa Utetezi uliokuwa unaongozwa na Method Kimomogolo na Albert Msando ulidai kuwa Ndessamburo yuko nje ya nchi kwa matibabu na anatarajiwa kurejea  nchini Octoba 17 mwaka huu.

Kimomogolo aliieleza mahakama hiyo kuwa kupitia ujumbe walioupata
(Email) ambayo imeonyesha tarehe hiyo ya kurudi kwa mbunge huyo baada ya kupatiwa matibabu na kuwa taarifa hiyo wameiwasilisha mahakamani hapo na kwa Wakili wa Serikali.

Awali shauri hilo liliahirishwa Agosti 26 mwaka huu kutokana na
Ndesamburo na Josephine kutokufika mahakamani hapo ambapo ilidaiwa
kuwa Mbunge huyo amekwenda kwenye matibabu nchini Uingereza ambapo kwenye barua ya ruhusa  iliyotolewa na Spika wa Bunge, Anna Makinda ambayo ilikuwa haionyeshi tarehe ya ya kurudi nchini.

Kimomogolo alidai kuwa kwa upande wake Mchumba wa Dk. Slaa Josephine Mashumbusi, ameshindwa kufika mahakamani hapo kutokana na taarifa iliyotolewa na Daktari anayemhudumia kuwa anatakiwa mapumziko ya wiki mbili hadi Octoba 2 mwaka huu.

Wakili huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa kutokana na mazingira hayo
wanaiomba mahakama hiyo usikilizwaji wa  awali wa kesi hiyo uwe Octoba 21 mwaka huu. Kufuatia maelezo hayo wa Wakili wa Utetezi, wakili wa Serikali alisema kuwa upande wa jamhuri haupingani na rai hiyo na kuukumbusha upande wa utetezi kuwa amri ya mahakama, ilionyehsa kuwa kesi hiyo usikilizwaji wake wa awali ulitakwia kuwa Machi 25 mwaka huu.

Alisema kuwa ni zaidi ya miezi sita imepita tangu kesi hiyo kutakwia
kuanza kusikilizwa il akutokana na baadhi ya watuhumiwa kutokufika
mahakamani shauri hilo limekuwa likikwama kuanza kusikilizwa.

Pande aliukumbusha  upande wa utetezi kuwa shauri lolote  linapokuwa
mahakamani linatakiwa kuendelea na siyo kukwamwishwa na sababu
zisizokuwa za msingi. Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Hakimu Charles Magesa alisema amekubaliana na ombi la wakili Kimomogolo la kuahirisha kesi hiyo hadi Octoba 21 mwaka huu kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa (Arusha Mjini)
Godbless Lema, Joseph Selasini (Rombo), Derick Magoma, Samson
Mwigamba, John Materu, Peter Marua, Mathias Valerian, Dadi Igogo, Aquiline Gervas, Nai Steven, Walter Mushi, Daniel Titus, Juma Samweli, Richard Mtui na Basil Lema.