Na Mwandishi Wetu,Addis Ababa
MATAIFA zaidi ya Afrika yamesaini mkataba wa kujiunga na mchakato wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) wakati wa kikao cha wakuu wa nchi za Umoja wa Afrika (AU) zinazoshiriki katika tathmini ya APRM mjini hapa.
Mkutano wa wakuu wa nchi zinazoshiriki APRM ulifanyika Jumamosi ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kwa kikao cha wakuu wa nchi za AU ambapo Rais Jakaya Kikwete aliongoza idadi ya Marais wa Afrika waliohudhuria mkutano huo wa APRM.
Nchi mpya zilizosaini mkataba wa kukubali kukaguliwa kiutawala bora chini ya APRM ni Niger, Cape Verde, Chad, Tunisia na Guinea ya Ikweta, hivyo kufikisha idadi ya nchi 36 kati ya 54 wanachama wa AU walioamua kujiunga na mchakato wa APRM.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania, Hassan Abbas, APRM huipa nchi fursa kuanzisha taasisi yake ya ndani kwa lengo la kuwapa wananchi fursa ya mara kwa mara kuitathmini nchi yao katika utawala bora, kisha tathmini hiyo kuhakikiwa na wataalamu wengine kutoka nchi za Afrika kwa lengo la Afrika kama Bara na kila nchi kujikosoa ili baadaye kujisahihisha.
Akizungumza mjini Addis mara baada ya mkutano huo wa marais, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, RehemaTwalib alisema mkutano huo ulikuwa wa mafanikio na viongozi hao walipitisha maazimio mengi ikiwemo kuiimarisha APRM ili kuwa taasisi kamili ya Umoja waAfrika.
Rais Kikwete aliunganana marais wengine akiwemo Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Waziri Mkuu wa Ethiopia,Melesi Zenawi na Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika mkutano huo.
Mkutano huo pamoja namambo mengine pia ulijadili taarifa ya utekeleza wa hali ya utawala bora kwa nchiza Uganda, Burkina Faso na Algeria. Rais Abdulaziz Bouteflika wa Algeria aliwakilishwa na Waziri Mkuu wan chi hiyo, Ahmed Ouyahia.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizojiunga mapema tu tangu mchakato huo ulipoanzishwa mwaka 2003 kwa kusaini mkataba mwaka 2004, Bunge likauridhia mwaka 2005 na tayari ripoti iliyosheheni maoni ya Watanzania kuhusu utawala bora nchini imeshakamilika.