Nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki yasisistizwa kutumia Rasilimali zake

RAIS WA ZANZIBAR na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa mafanikio makubwa yanaweza kupatikana katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki iwapo zitatumia vyema rasilimali zake ilizonazo.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Uganda nchini Tanzania Mhe. Ibrahim Mukiibi, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zimejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi hali ambayo inatoa fursa nzuri katika maendeleo ya kiuchumi katika nchi hizo iwapo zitatumika vyema rasilimali hizo.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alisema kuwa hatua za uimarishaji wa miundombinu ya barabara katika nchi zilizomo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki una umuhimu wa pekee katika kurahisisha usafiri katika nchi hizo pamoja na kuimarisha sekta za maendeleo.
Alisema kuwa uimarishaji wa miundombinu ya barabara pamoja na aina nyengine za usafiri kati ya Tanzania na Uganda na nchi nyengine za Afrika Mashariki kutasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa ushirikiano kwenye sekta za maendeleo.
Alisema kuwa kwa upande wa Tanzania juhudi za makusudi zimekuwa zikichukuliwa katika kuhakikisha miundombinu ya mawasiliano hasa barabara zinaimarishwa ili kukuza sekta ya usafiri na usafirishaji kati ya nchi za Afrika Mashariki ikiwemo nchi ya Uganda.
Akizungumzia juu ya uimarishaji wa mashirikiano katika sekta ya biashara, Dk. Shein aliunga mkono wazo la Balozi Mukiibi la kuimarisha sekta hizo hasa katika maeneo ya mipakani ili kurahisishsa sekta hiyo ya usafiri kati ya Tanzania na Uganda.
Alisema kuwa juhudi za makusudi zinahitajika katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya kilimo kwa lengo la kuhakikisha chakula cha kutosha kinakuwepo ili kupambana na adui njaa katika nchi za Afrika Mashariki.
Dk. Shein alisema kuwa kumekuwa na mashirikiano na uhusiano mwema ambao ni wa muda mrefu kati ya Zanzibar na Uganda hasa katika uimarishaji wa sekta za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu umeimarika hali ambayo imepelekea Wazanzibari wengi kupata elimu nchini humo hasa katika Chuo Kikuu cha Makerere.
Katika maelezo yake Dk. Shein alimueleza balozi huyo kuwa atahakikisha nafasi aliyonayo ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar anaitumia vizuri kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu nchini sambamba na kutatua baadhi ya chagnamoto zilizopo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikiimarisha sekta zake za maendeleo nchini ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua za makusudi katika kupambana na umasikini sanjari na kutekeleza Dira ya 2020 pamoja na Malengo ya Milenia.
Nae Balozi wa Uganda nchini Tanzani Mhe. Ibrahim Mukiibia, alimueleza Dk. Shein kuwa Uganda inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo kati yake na Zanzibar pamoja na Tanzania kwa ujumla na kusisitiza kuwa nchi yake itaimarisha zaidi.
Alisema kuwa katika kuimarisha na kukuza zaidi ushirikiano na uhusiano uliopo kati ya nchi za Afrika mashariki hasa Uganda na Tanzania ipo haja ya kuimarisha miundombinu ya barabara kwa lengo la kurahisisha usafiri na usafirishaji bidhaa hasa kwa maeneo ya mpakani.
Alisema kuwa aina zote muhimu za usafiri zinahitajika kati ya nchi hizo na kusisitiza kuwa hata sekta ya biashara inaweza kuimarika iwapo sekta hiyo itafanyiwa kazi.
Alisema kuwa ipo haja ya kuiamrisha zaidi ushirikiano katika sekya ya elimu ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na utaalamu kati ya Uganda na Zanzibar.
Balozi Mukiibi, alimpongeza Dk. Shein kwa kuchaguliwa hivi karibuni kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na kusisitiza kuwa ana imani kubwa na uongozi wake huo katika chama chake hicho huku akimpongeza kwa hatua zake za kusimamia amani na utulivu uliopo nchini.
Aidha, Balozi huyo aliimpongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein kwa kusimamia na kuendeleza vyema shughuli za maendeleo kwa kuwa na mikakati madhubuti iliyowekwa na Serikali ya kuwaletea maendeleo wananchi wote wa Zanzibar.
Balozi huyo ameeleza kuwa licha ya kumaliza muda wake wa kazi nchini Tanzania lakini anatambua mashirikiano mazuri aliyoyapata kutoka kwa viongozi pamoja na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku akisisitiza haja ya kuimarisha mashirikiano ya kiutamaduni kwa pande zote mbili kutokana na kwenda sambamba.