Nchi za Afrika zashauriwa kuwaenzi diaspora

Akitoa mada kuhusu namna Bara la Afrika lilivyoimarisha taasisi na misingi ya utawala bora, Mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi za Siasa wa Chuo Kikuu cha Lagos, Prof. Adele Jinadu alisema katika utafiti wake kutokana na kushiriki katika tafiti tathmini kadhaa za nchi za Afrika chini ya APRM umeonesha kuwa suala la diaspora hasa haki zao za kupiga kura bado ni changamoto.

Na Hassan Abbas, Addis Ababa

Viongozi wa Afrika wametakiwa kuenzi mchango wa Waafrika walioko nje ya Bara na walioko nje ya nchi zao si tu kwa kutambua mchango wao kiuchumi bali kuwapatia haki za kiraia na kisiasa ikiwemo kupiga kura.
Wito huo umetolewa jijini hapa wakati wa mkutano wa siku mbili ulioandaliwa kutafakari miaka kumi ya Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) ambao Tanzania ni mwanachama.
Akitoa mada kuhusu namna Bara la Afrika lilivyoimarisha taasisi na misingi ya utawala bora, Mhadhiri kutoka Idara ya Sayansi za Siasa wa Chuo Kikuu cha Lagos, Prof. Adele Jinadu alisema katika utafiti wake kutokana na kushiriki katika tafiti tathmini kadhaa za nchi za Afrika chini ya APRM umeonesha kuwa suala la diaspora hasa haki zao za kupiga kura bado ni changamoto.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizotambua mchango wa diaspora na tayari imeanza jitihada kubwa za kutambua mchango wao ikiwemo kuunda idara inayoshughulikia masuala yao kwenye Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.  
Akitoa maoni yake mmoja wa washiriki katika semina hiyo alibainisha kuwa Afrika ina aina tatu ya diaspora ambao ni wale waliochukuliwa kwenda nchi za nje wakati wa utumwa, diaspora waliohamia wenyewe nchi za nje ya Afrika kusaka maisha hasa katika miaka ya 1980 na 1990.
Alilitaja kundi latatu kuwa ni la diaspora wanaoishi nje ya nchi zao lakini ndani ya Afrika. Akashauri kuwa ni vyema Mpango wa APRM ukalifanyiakazi tatizo la diaspora na kutoa mapendekezo kwa nchi za Afrika juu ya nini cha kufanya.
 Kwa upande wake Prof. Alinah Segobye alisema licha ya mchango wa diaspora katika nyanja za uchumi wanaweza pia kutumiwa ipasavyo kusaidia uwekezaji katika elimu Barani Afrika.