Na James Gashumba, EANA-Arusha
SHIRIKISHO la Kisiasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) linaweza lisifikiwe iwapo nchi tano wananchama wa jumuiya hiyo hazitatekeleza kikamilifu itifaki za shirikisho hilo zilizokwishakubaliwa, wataalamu wametahadharisha.
Wajumbe wa mkutano wa pili wa Mdahalo wa Shirikisho la EAC walisema itafaki ambazo zinatakiwa zitekelezwa kikailifu ni pamoja na Soko la Pamoja, uliotiwa saini 2009 na Umoja wa Forodha uliotiwa saini 2004 na kuanza kazi rasmi 2005.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika hivi karibuni mjini Dar es Salaam, Profesa Gilbert Khadiagala wa Chuo Kikuu cha Pretoria alisema, Shirikisho la Kisiasa la EAC linaweza kupatikana baada ya kufanikiwa katika uchumi wa kanda, ambao utapatikana kufuatia utekelezaji halisi wa itifaki za kiuchumi zilizotajwa.
“Mtangamano wa kiuchumi ndiyo msingi wa ushirikiano wa kisiasa na ushirikiano wa kisiasa unasaidia katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, hivyo mambo hayo mawili yanategemeana,” Prof. Khadiagala alisema.
Aliongeza “Mtangamano wa uchumi na kisiasa unapatikana tu iwapo lengo kuu la kanda nzima ni kukana utaifa na kuwekeza kwenye taasisi kuu za kikanda.”
Alifafanua kwamba ili EAC iweze kufikia hatua ya shirikisho la kisiasa nchi wananchama hazinabudi kujitoa toka ushitikiano baina ya nchi na kuingia kwenye ngazi nyingine iliyo zaidi ya utaifa.
Alizitaja changamoto zilizopo kufikia shirikisho la kisiasa kuwa ni pamoja na kutokuwa na mijadala ya kutosha kuhusu vikwazo vilivyopo na hali ya kutoaminiana juu ya faida za kiuchumi.
Naye Profesa Sam Tulya-Muhika wa Chuo Kikuu cha Makere, alisema ni muhimu kuondoa vikwazo vyote vya kibishara katika kanda katika harakati za kufikia shirikisho la kisiasa. Mkutano huo ulihudhuriwa na asasi za kiraia, wasomi, wanasiasa na maafisa waandamizi wa serikali kutoka nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Wajumbe wa mkutano huo pamoja na mambo mengine walikubaliana kwamba ipo haja ya kuongeza wigo wa washiriki katika midahalo inayohusu shirikisho la kisiasa kwa kujumuisha wadai zaidi, sekta nyingi zaidi na makundi mengi zaidi.
Shirikisho la Kisiasa la EAC itakuwa ni hatua ya nne na ya mwisho ya mtangamano wa EAC ikiwa umetanguliwa na Soko la Pamoja, Umoja wa Forodha na Umoja wa Fedha.