Nchemba Kuwapa Yanga Kesho Kombe Lao Taifa

mwigulu1

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba Madelu kesho Jumamosi Mei 14, 201 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya Ndanda na Young Africans katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali ya Nchemba ambaye atakabidhi Kombe kwa Yanga ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2015/16, wageni wengi maalumu watakaokuwa kwenye mchezo huo ni Mkurugenzi wa Vodacom, Ian Ferrao sambamba na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na viongozi wengine wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi ya Kuu Tanzania Bara (TBLB).

Mchezo huo utafanyika kwa baraka za TPLB baada ya maombi ya Young Africans kukubaliwa na Ndanda ambao watakuwa wenyeji wa mchezo huo utakaoanza saa 10:00 jioni.

Mara baada ya mchezo huo, Mabingwa Young Africans watapewa Kombe la ubingwa, medali na fedha Sh 81,345,723; Mshindi wa Pili Sh 40,672,861; Mshindi wa Tatu Sh 29,052,044 na Mshindi wa Nne atazawadiwa Sh 23,241,635.

Mcehzaji Bora atapewa Sh 5,742,940 sawa na Mfungaji Bora wa Ligi na Kipa bora wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Vodacom, Bia ya Kilimanjaro, Azam, Startimes na NHIF. Mwamuzi Bora atazawadiwa Sh 8,614,610 saw na Kocha Bora wakati timu yenye nidhamu itavuna Sh 17,228,820.

Young Africans ndiyo iliyoomba kwa Ndanda kadhalika TPLB kuomba ridhaa ya mchezo huo kufanyika Dar es Salaam kwa kuwa inatarajiwa kusafiri kwa ndege Jumapili kwenda Angola kwa ajili ya mchezo wa marudiano dhidia ya Sagrada Esperanca ya Angola utakaofanyika ama Mei 17 au 18, mwaka huu.

Barua ya Bodi ya Ligi kwa TFF imesema kwamba Young Africans watatumia mchezo huo ambao Ndanda itakuwa mwenyeji kupokea taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara litakalotolewa na Nchemba ambaye mara nyingi anaonekna uwanjani.

Kanuni ya pili ya Ligi Kuu Bara toleo la 2015/16 imeeleza wazi kuwa, “Katika mazingira maalumu, timu inaweza kucheza mchezo wake wa nyumbani katika uwanja mwingine endapo kuna sababu nzito na za msingi, utambulisho wa uwanja katika mazingira haya pia unawajibika kufanywa katika kipindi cha uthibitisho wa kushiriki ligi au kwa maombi maalumu kwa TPLB,” inasehemu kanuni hiyo. Kwa kuzingatia kanuni hiyo na sababu za yanga ambazo Ndanda na Bodi wameona kuwa ni nzito wamekubaliana kucheza mchezo huo Dar es Salaam.

Tayari Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ameipongeza timu ya soka ya Young Africans kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo baada ya kufanya hivyo msimu uliopita wa mwaka 2014/2015.

Hii ni mara ya 26 kwa Young Africans ambayo kwa sasa inacheza mashindano ya kuwania kutwaa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kutwaa taji hilo tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1965. Simba inafuatia katika rekodi hiyo baada ya kulitwaa taji hilo kwa mara 18.

“Nichukue nafasi hii kuipongeza Young Africans kwa ubingwa. Pia nizipongeze timu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kushiriki na kufanya msimu wa Ligi Kuu Bara ya Vodacom 2015/16 kuwa wenye mafanikio,” amesema Rais Malinzi baada ya Young Africans kufikisha pointi 71 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine 15 zilizoshiriki ligi hiyo.