Na Mwandishi wa Thehabari, Dodoma
CHAMA cha NCCR Mageuzi kupitia mbunge wao wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila kimetoa tuhuma nzito za rushwa zinazofanywa na baadhi ya wabunge na mawaziri na kimedai kinawajua viongozi hao kwa majina.
Kafulila ametoa tuhuma hizo leo akichangia Mpango wa Maendeleo ya Miaka Mitano kuanzia 2011/2016 ambapo alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa mpango huo bado kuna matatizo makubwa na mengine yanatokana na baadhi ya wabunge kuchukua rushwa kwa wananchi.
Alisema kuwa majina ya baadhi ya wabunge ambao wanachukua rushwa anayo na kwamba hali hiyo inasababisha kuwepo na utawala ambao unaonekana kuendeshwa kifisadi jambo ambalo haliwezi kuvumulika.
Hata hivyo Kafulila wakati anazungumzia tuhuma hizo za rushwa aliaamua kutaja majina ya wabunge wawili (majina tunayo) kwa madai kuwa aliwaona wakiomba rushwa kwa wananchi na kusisitiza kuwa kwa mfumo huo nchi haiwezi kuendelea kama kuna viongozi wanajihusisha kwa matukio ya rushwa.
Mbunge huyo kijana katika kuongeza msisitiza wa tuhuma ambazo amezitoa bungeni, alisema kuwa baadhi ya wabunge ambao wanajihusisha na rushwa wapo katika bungeni na wanaendelea na vikao vya Bunge la bajeti.
“Wabunge wanaochukua rushwa wapo humu ndani wengine.Kuna matatizo mengi lakini kubwa ni la kimfumo ambao unatokana ufisadi.Kwa mazingira hayo nchi hawezi kwenda,hili suala la kuomba rushwa,”alisema Kafulila.
Mwenyekiti wa Bunge jana jioni, George Simbachawene pamoja na tuhuma hizo bado aliamua kumuomba Kafulila akae chini kwa kuwa muda wake ulikuwa umekwisha kuchangia.
Hata hivyo kutokana na muda wa Kafulila kwisha baadhi ya wabunge akiwemo Felix mkosamali wa Jimbo la Muhambwe kupitia NCCR-Mageuzi alitaka kujua hatua gani ambazo zitachukuliwa kwa wabunge ambao wametajwa kuhusika na rushwa.
Kafulila akizungumzia kuhusu mpango wa maendeleo ya taifa, alisema kuna mambo mengi ambayo yanatakiwa kuangaliwa kwa kina kuhusu maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati thabiti ya kuhakikisha unafanikiwa kwa maslahi ya nchi.
Alisema kuwa kwa bahati mbaya Tanzania imekuwa na mipango mizuri kwenye vitabu lakini linapofika suala la utekelezaji mambo yanashindaka na madhara yake ni kwamba unaweza kuwa na mipango mizuri lakini hakuna mafanikio zaidi ya maisha ya wananchi kuendelea kuwa magumu.
Alishauri mipango ilenge kukuza kilimo angalau kwa asilimia 10, ili Watanzania wataweze kufaidika na uchumi wao, kwani uchumi umekuwa ukikua lakini hauwafikii Watanzania, huku asilimia 50 wakiwa bado masikini.
“Miaka 50 ya uhuru bado tunaendelea kuwa tegemezi, kampuni za simu watanzania takribani milioni 20 ni wateja wao je utafiti umefanyika na kodi zinalipwa za kutosha?, jambo linalosikitisha ni namna ambavyo viongozi tunakuwa na dhamira ya kusimamia hii bajeti,”alisema.