NCCR-Mageuzi wampongeza JK mchakato wa Katiba Mpya

Mazungumzo ya Rais Kikwete na viongozi wa NCCR-Mageuzi

Rais Kikwete akifanya mazungumzo na uongozi wa NCCR-MAGEUZI Ikulu Dar es Salaam. PICHA ZOTE NA IKULU

Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha National Convention for Construction and Reform-Mageuzi (NCCR-Mageuzi) kimempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kusimamia suala la Katiba vizuri na kwa umakini mkubwa.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia ametoa pongezi hizo leo jioni alipofika Ikulu, akiongoza ujumbe wa viongozi wenzake sita(6), kuja kujadili suala la Katiba Mpya ya Tanzania.

“Tunakupongeza kwa kusimammia suala la Katiba vizuri, ni suala zito ambalo litatupa uhai vizazi na vizazi vijavyo”. Amesema kama utangulizi wa ujio wao Ikulu. Upinzani sio uadui, tunahitaji kufanya marekebisho ya Katiba kwa amani na hoja bila kuvuruga amani yetu,” Mbatia amesema na kuongeza kuwa “suala la Katiba linahitaji ushirikiano wa pamoja kwa nia njema, kwani taifa hili ni letu sote” ameeleza.

Akiwakilisha hoja ya NCCR-Mageuzi kwa Rais Kikwete, Mkuu wa Idara ya Sheria wa NCCR-Mageuzi Dk. Senkondo Mvungi amesema, NCCR – Mageuzi inatambua ukubwa wa jambo hili la wa Tanzania kupata Katiba.
“Ni jambo kubwa sana, wewe ndiyo Rais wa kwanza kutengeneza sheria ya kupata katiba mpya na kuanzisha Mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Kikao cha leo cha Rais na viongozi wa NCCR-Mageuzi ni mwendelezo wa jitihada za Rais Kikwete, kusikiliza, kuchukua maoni na mawazo ya wadau mbalimbali kutoka vyama vya siasa, asasi za kijamii na makundi mbalimbali katika kuelekea mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Tanzania.

Rais amesema kuwa nchi hii inayo Katiba ambayo imelilea vizuri na kulifikisha Taifa la Tanzania hapa lilipo, lakini pia Taifa linahitaji Katiba inayoendana na wakati na itakayoweza kulilea Taifa hili kwa miaka mingi ijayo.

Mara baada ya kumaliza kikao na viongozi wa NCCR-Mageuzi, Rais Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ikiwa ni mwendelezo wa mazungumzo yao yalioanza mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka 2011, kuhusu Katiba Mpya ya Tanzania.

Katika mazungumzo haya na Vyama vya Siasa Rais amesisitiza kuwa lengo la mazungumzo haya yote ni kuhakikisha kuwa hatimaye Watanzania wote watakiri kuwa Katiba Mpya ni yao wote na hatimaye ifikapo mwaka 2015 nchi iweze kufanya uchaguzi wake na Katiba Mpya.