Na Joachim Mushi, Dar es Salaam
CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema taarifa zinazozagaa kuwa chama hicho kimejitoa ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) hazina ukweli wowote na kwamba hawawezi kujitoa kwa kuwa wao ni miongoni mwa waasisi wa ushirikiano huo uliozaliwa na mchakato wa Katiba mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Nderakindo Kessy alisema chama hicho hakiwezi kujitoa UKAWA bila sababu za msingi na taarifa zinazozagaa kuwa wamejitoa ni za uzushi na propaganda za kisiasa ili kuudhohofisha ushirikiano huo.
Alisema chama cha NCCR-Mageuzi ni kitovu cha UKAWA kwani UKAWA ilizaliwa katika Bunge la Katiba, ambapo Katiba mpya ni tunda la NCCR-Mageuzi hivyo haiwezi kujitoa bila ya maamuzi ya Halmashauri Kuu ambayo ndiyo iliyoridhia chama kushiriki katika ushirikiano huo.
“…UKAWA tunaamini ni tunda la NCCR-Mageuzi kwa hiyo itakuwa ni kitu cha ajabu tukaacha tunda letu ambalo tumelipigania kwa miaka 24 tukalitupa leo…kwa hiyo tunaomba wanachama wa NCCR-Mageuzi watulie tunafuatilia hilo na wanajua kabisa chama chetu kinafuata taratibu wanasheria na kitengo cha sheria, katiba na ilani wanafanyia wanafanyia uchunguzi juu ya taarifa hizi…,” alisema Bi. Kessy.
Wakati huo huo chama hicho kimetangaza majimbo 19 ya uchaguzi Mkuu ambayo watasimamisha wagombea kwa makubaliano na ushirikiano wao wa UKAWA. Alisema majimbo hayo ambayo wameafikiana na ngazi ya UKAWA ni 19 kati ya majimbo 265 ya ushirikiano wao wa UKAWA.
Aliyataja majimbo hayo kuwa ni pamoja na Jimbo la Kasulu Vijijini, Kasulu Mjini, Jimbo la Buyungu, Jimbo la Muhambwe, Jimbo la Kigoma Kusini, Jimbo la Manyovu, Jimbo la Mwanga, Jimbo la Vunjo, Jimbo la Mtwara Mjini, Jimbo la Mufindi Kusini, Jimbo la Gairo, Jimbo la Kibakwe, Jimbo la Mpwapwa, Jimbo la Mtera, Jimbo la Ngara, Jimbo la Nkenge, Jimbo la Mbinga Mjini, Jimbo la Serengeti na Jimbo la Ileje.
“…Hayo ndio majimbo ambayo kati ya majimbo 269 ndani ya UKAWA tumekubaliana NCCR-Mageuzi itasimamisha wagombea katika majimbo 19 niliyoyataja,” alisema Kaimu Katibu Mkuu huyo wa chama cha NCCR-Mageuzi.