Na Dotto Mwaibale
MWENYEKITI wa Chama cha Walaji na Tiba Tanzania , Elias Nawera, ameitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutatua changamoto ya bei kubwa ya dawa za binadamu wanayotozwa Watanzania. Nawera alisema sera ya afya inasema kila mtu ana haki ya kupata huduma za afya kwa bei nafuu, lakini bado Watanzania wengi wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kununua dawa kwa bei kubwa.
“Tunaomba Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii aingilie kati suala hili, wanaoteseka kwa kiwango kikubwa ni watu wa kipato cha chini.
Nimesema hivi baada ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Baraza la Famasia kushindwa kulitafutia ufumbuzi suala hili.
Alitoa kauli hiyo Dar es Salaam juzi, wakati akizungumza na wanahabari, ambapo alifafanua kuwa, amefikia hatua hiyo baada ya kubaini mzigo mkubwa wa gharama za matibabu wanaobebeshwa Watanzania.