IMEELEZWA kuwa gharama kubwa za usafiri wa anga nchini zitapungua pale Serikali itakapoliwezesha Shirika la ndege Tanzania (ATCL), kuwa na ndege zake. Akizungumza mara ya kukagua kiwanja cha ndege cha Nduli Mkoani Iringa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema kwa mwaka wa Fedha 2016/17 kiasi cha bilioni 500 kimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa ndege tatu.
“Nauli za usafiri wa anga zitashuka hivi karibuni pale ndege tatu tulizoziagiza zitakapoanza kutoa huduma ya Usafiri hapa nchini hivyo niwatoe hofu watumiaji wa usafiri wa anga”. Alisema Profesa Mbarawa.
Prof. Mbarawa amemuagiza Meneja Uwanja wa ndege wa Nduli Mkoani Iringa Bi. Hana Kibupile kuhakikisha kwamba uwanja wa ndege wa Iringa unafanya kazi katika viwango vinavyokubalika kimataifa ili kuvutia wasafiri wengi wanaoelekea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kutumia uwanja huo na hivyo kukuza uchumi wa Iringa.
“Uwanja wa ndege wa Iringa ni miongoni mwa viwanja 11 ambavyo tutavifanyia ukarabati hivi karibuni hivyo jukumu lenu ni kutoa huduma inayokidhi viwango.”amesisitiza Prof. mbarawa.
Waziri huyo wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amesema Serikali itaupanua uwanja wa ndege wa Iringa hivyo wote waliovamia eneo la uwanja huo waondoke mara moja kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao na wale watakaochukuliwa maeneo yao Serikali itawafidia.
Naye Meneja wa uwanja wa ndege wa Iringa Bi. Hana Kibupile amemuomba Waziri Prof. Mbarawa kuupa uwanja huo gari jipya la zimamoto ili kuuwezesha uwanja huo kufanya kazi katika viwango vinavyokubalika.
Idadi ya abiria wanaotumia uwanja wa ndege wa Nduli imeongezeka kutoka abiria 4405 mwaka 2011 hadi 8375 mwaka 2015 na hivyo kuongeza uchumi wa Mkoa wa Iringa.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua barabara ya Iringa –Kilolo yenye urefu wa KM 35 na kusisitiza kwamba Serikali imepanga kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa KM 28 zilizobaki.
Imetolewa na kitengo cha Mawasiliao Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.