*Asema hatishiki kusimamia haki
Katibu wa NEC ya CCM wa Itikadi na uenezi, Nape Nnauye amesema CCM sio kichaka cha kujifichia mafisadi na viongozi wabovu na
wabadhilifu na kwamba wanaodhani watafanikiwa kukigeuza chama hicho kichaka wanajidanganya.
Bwana Nape aliyasema hayo jijini Mwanza leo wakati akihutubia mkutano mkubwa na wa aina yake kwenye viwanja vya Igoma Sokoni ulioandaliwa na Chama hicho katika mwendelezo wa ziara ya baadhi ya viongozi wa kitaifa wa CCM kanda ya ziwa iliyoanza tangu juzi.
Akitumia mifano kadhaa ya bibilia na qurwani bwana Nape alisema hata
Bwana Yesu alipokuta wafanya biashara wanageuza nyumba ya baba yake pango la walanguzi aliwakemea na kuwafukuza, hivyo naye anachofanya ni kusafisha Chama ili kisigeuzwe kichaka cha kujifichia waovu.
“Yesu alikwenda hekaluni na kuwaambia wafanya biashara nyumba ya baba yangu itakuwa nyumba ya sala na si pango la wanyang’anyi, akapindua meza zao na kuwafukuza kwa ukali, leo Nape akikemea maovu ndani ya chama mnataka kumtoa roho? Sitishiki Mungu yuko upande wangu na ndio maamuzi ya Chama changu nami nayaamini,” alisisitiza Nape.
Aliendelea kusema kwa mifano kadhaa,ambapo aliwashangaa baadhi ya
viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya kujilimbikizia mali
wakiwajibika serikalini wanaenda kujificha kwenye chama, akihoji kuwa
tabia hiyo ni kukigeuza chama kuwa kichaka cha waovu na hivyo
kukifanya chama kupoteza imani yake kwa wananchi.
“Kama wanaoonekana serikalini hawafai, au kwenye mashirika ya umma wameshiriki kuyaua, hapa Mwanza mfano mzuri ni waliokifikisha chama cha ushirika Nyanza kilipo leo, halafu hao ndio tunawakumbatia na kuwapa nafasi kwenye Chama nani atatuamini?” alihoji Nape.
Akasema alishwahi kutangaza mahali pengine na hivyo anarudia Mwanza
kuwa wale walioshiriki kwa namna moja ama nyingine na hujuma kwa Chama cha Ushirika Nyanza uchaguzi wa mwakani wa CCM wasichukue fomu za kugombea nafasi yeyote kwani matendo hayo yanatosha kuwapotezea sifa ya kuwa viongozi wa Chama.
Alisema ni sera ya CCM kujenga na kuimarisha ushirika nchini, hivyo
yeyote aliyeshiriki kuhujuma chama cha ushirika popote nchini ni
msaliti kwa Chama na hivyo hastahili kuwa kiongozi kwenye Chama Cha
Mapinduzi.
” ndugu zangu wana Mwanza nani asiyejua jinsi Nyanza ilivyokuwa msaada kwa wakulima wa Pamba kanda ya ziwa? Ikizingatiwa kuwa ni sera ya CCM kuimarisha ushirika, sasa aliyeshiriki kuifikisha Nyanza ilipofika timwiteje kama sio msaliti?.. Aliuliza Nape na kuitikiwa na vijana,” wavue magamba hao!!”
Huku akishangiliwa kwa nguvu na wafanya biashara wadogowadogo jijini
Mwanza, Nape alihoji utaratibu unaotumiwa na majiji mengi
kushughulikia swala la Machinga na mama na baba lishe nchini, kuwa
inatumika nguvu kubwa sana pengine kuliko inavyotakiwa ikiwemo
kuwadhulumu mali zao jambo analodai si sawasawa.
“Naambiwa na vijana hapa, mgambo mnapowafukuza hawa vijana mnachukua hata mali zao kidogo zinazowafanya waishi na wakati mwingine mnadaiwa kugawana wenyewe mali hizo, huku ni kutengezeana umasikini bila sababu, lazima tubadilike, hii si sawa” alilalamika Nape.
Alishauri utumike utaratibu bora zaidi kushughulikia swala la machinga
nchini kote bila kusababisha umasikini zaidi kwa mtaji mdogo
waliodunduliza wafanya biashara wadogo hao.
Alisema hata kina mamantilie wanajitafutia kwa tabu sana riziki yao ya
siku, lakini bahati mbaya pengine wanakosea utaratibu wa mahali pa
kukaa na kufanya biashara zao kisha mgambo wanapokwenda na kuchukua mpaka chakula chao, jambo linaloharibu mtaji wao kabisa, inakuwa sawa na kuwarudisha nyuma kabisa kuanza sifuri wakati walishapiga hatua.
Alisisitiza kuwa si kwamba anatetea uvunjifu wa sheria, lakini
anasisitiza isitumike nguvu kiasi cha kupelekea kuharibu na kupoteza
kabisa mitaji ya hawa wajasiriamali wadogo wadogo.
Aliitaka manispaa ya Mwanza kutenga maneo vizuri kwa kuzingatia sheria nataratibu bila upendeleo lakini kwa kuwashirikisha wafanya biashara wadogo wadogo wenyewe ili pasitokee tena mivutano kama iliyowahi kutokea nyuma na hivyo kusababisha hasara kubwa kwa uchumi wa Mwanza.
“kaeni nao, hawa ni Watanzania mjadili namna bora ya kushughulikia
migogoro hii. Hebu fikiri ungekuwa unafanya hivyo kwa ndugu yako wa
damu au mzazi wako ungejisiaje? Tubadilike ndugu zangu,” alishauri
Nape.
Ziara hiyo ya viongozi wa CCM taifa kanda ya ziwa itaendelea kwenye
wilaya ya Geita na Ukerewe, lengo likiwa ni kuamsha ari ya wanachama
hasa baada ya uchagizi mkuu wa mwaka jana ambapo CCM inaonekana kuto fanya vizuri kama ilivyokua mwaka 2005.
Pamoja na Nape na Nchemba, msafara huo pia umeambatana na Mhe.
Livingstone Lusinde ambaye ni Mbunge wa Mtera na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, pamoja na Katibu Msadizi Mkuu wa Idara ya Itikadi, Sixtus Mapunda.