Na Mwandishi Wetu, Igunga
KATIBU wa NEC ya CCM, Nape Nnauye leo ametinga katika jimbo la Igunga mkoani Tabora na kuzusha taharuki kwa viongozi wa CHADEMA. Nape alifika Inguga saa sita mchana na kwenda kutoa pole familia ya mtoto Peter Ezekiel ambaye alifariki papo hapo baada ya kugongwa na lori la mizigo, alipojaribu kukatiza barabara akitokea katika umati wa watu waliokuwa wakisubiri msafara wa mgombea wa
CCM katika jimbo hilo.
Kufuatia msiba huo, CCM ilisimamia taratibu zote hadi mazishi ambapo katika mazishi yaliyoyanyika juzi nye kidogo ya mji wa Igunga, CCM ilitoa rambirambi ya sh. milioni moja, huku CHADEMA ambao nao wameweka mgombea jimboni hapa wakitoa sh. 120,000.
Nape aliwasili mjini Igunga saa sita mchana na kukatika safari yake kwenda moja kwa moja nyumbani kwa wazazi wa marehemu Ezekiel ambapo alitoa pole na kutoa ubani wa kiasi cha fedha ambacho hakupenda kukitaja.
“Nisingependa kusema mengi hapa, lakini naomba niwaombe kuwa watulivu wakati huu mgumu kwa msiba wa mtoto wetu mpendwa. Hii ni mipango ya Mungu, nimeona nipite hapa kuwapa pole kwa kuwa nilipata habari za msiba huu”, alisema Nape.
Msemaji wa familia ya mtoto huyo, Joseph Mlewa alisema, familia hiyo imefarijika kwa namna CCM ilivyoshughulikia msiba mwanzo hadi mwisho na kwamba angeomba moyo huo uendelee kila inapopata fursa. “Tangu msiba huu utokee wa Ezekiel CCM wametusaidia sana, wamesimamia hadi mwisho wa mazishi, tunasema asanteni sana CCM na tunawaombea kila la kheri kwa kila jambo mtakalofanya”, alisema.
Wakati Nape akitoa pole Mratibu wa kampeni za CHADEMA Mwita Waitara alionekana akifanya doria jirani na nyumba ya familia hiyo iliyopo mita 500 kutoka barabara kuu ya Singiga-Igunga.
Baada ya Nape kutoka kutoa pole alifika kwenye baa moja iliyopo jirani ya nyumba ya familia hiyo ambako pia walikuta vijana kadhaa na kuwasalimia, lakini katika eneo hiyo pia alikuwepo baunsa mmoja mmarufu wa CHADEMA kutoka Dar es Salaam, ambaye inadaiwa alitumwa kumfuatilia Nape.
Vyama vya CCM na CHADEMA ni miongoni mwa vyama kadhaa vilivyoweka wagombea wake katika uchaguzi mdogo wa Igunga ambao umepangwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu, baada ya kampeni zitakazochukua takribani mwezi moja kuanzia keshokutwa.