Na Bashir Nkoromo, Singida
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye ameshushia kilio tena kwa CHADEMA baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Singida Mjini, Nakamia John kukamia CCM. Nakamia ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu na Kamati Kuu ya Taifa ya CHADEMA, alitangaza kuhamia CCM na kukabidhi kadi yake ya CHADEMA kwa Nape katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani za CCM, Kata ya Urughu, jimbo la Iramba Magharibi mkoani hapa.
“Kama unakumbuka Mheshimiwa Nape, mimi ndiye nilikuvalisha gwanda la CHADEMA ulipokuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wetu mkuu kule Dar es Salaam, leo hii nimeamua niwe nawe katika chama makini CHama Cha Mapinduzi,” alisema Nakamia na kuongeza.
“Ukiwa nje ya CHADEMA unaweza kudhani ni chama makini sana, lakini ni chama cha udikteta ukiokithiri, kisicho na utaratibu unaoeleweka, chenye viongozi wa ngazi za juu ambao wanapenda kila wanalotaka liwe hata kama haliwezekani.”
Aliwataka Watanzania ambao bado wanadhani CHADEMA kina manufaa kuachana nacho haraka wasiendelee kugeuzwa mtaji wa maandamano ambayo alisema viongozi wa chama hicho huyapanga kwa lengo la kukusanya fedha kwa manufaa yao.
“Ninyi mnadanganywa kila siku eti nguvu ya umma, kumbe mnapumbazwa na kuacha kufanya kazi za maendeleo badala yake wanawapanga katika maanadamano, wanawapiga picha za video kisha wanapeleka kwa wafadhili kuombea fedha za kula wao ninyi mkiendelea kufa njaa”, alisema Nakamia.
Akimpokea, Nape alimpongeza na kuwataka Watanzania wengine kuiga alivyofanya Nakamia akisema kwamba kila anayekiunga mkono CHADEMA asidhani kuwa atapata manufaa yoyote kimaendeleo.
Akimnadi mgombea Udiwani wa Kata ya Urughu, Simon Tyosela, Nape aliwataka wakazi wa Kata hiyo kuhakikisha wanampigia kura mgombea huyo wa CCM ili aweze kusimamia miradi yote iliyopangwa kutekelezwa katika eneo lao.
Nape alionya wananchi kutofanya makosa, akisema endapo wataacha kumchagua mgombea wa CCM wakampigia wa CHADEMA watambue kwamba wamekataa maendeleo kwa kuwa yale yote yaliyopangwa kutekelezwa yapo ndani ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi kinachotawala.
Uchaguzi mdogo unafanyika kwa lengo la kukidhi taratibu na sheria tu za nchi, lakini kimsingi hakuna kinachoweza kubadilishwa katika mipango ya maendeleo.
“Baada ya uchaguzi mkuu mwaka jana, wananchi walichagua ilani ya kijani (ya CCM) kwamba ndiyo itekelezwe kwa miaka mitano hadi uchaguzi mkuu mwingine, kwa vyovyote vile anayefaa kupewa kujumu kusimamia lazima awe wa CCM”, alisema Nape.
“Wewe unatambua kuwa sera zinazotekelezwa kwa sasa hadi miaka mitano ni za CCM na mipango yote iliyopo inatekelezwa chini ya ilani hiyo, unachagua mgombea mwenye ilani nyingine ambayo haina kazi, unataka kusimamisa au kuendeleza maendeleo kweli?” alihoji Nape.
Alisema anao uhakika kwamba mgombea wa CCM taibuka na ushindi na alichokuwa akifanya juzi, si kuzindua tu kampeni bali kuandaa sherehe za mgombea huyo kutawazwa kuwa diwani wa kata hiyo.
“CHADEMA walishashindwa hata kabla ya uchaguzi kufika, Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zitto Kabwe alishaliona hilo mapema ndiyo maana hakuweza kuja kuzindua kampeni za chama hicho hapa kama alivyokuwa amewaahidi.” alisema Nape na kuongeza.
“Zitto aliposikia tu kuwa mimi nitakauja hapa akaona basi biashara imeingia ruba, akaamua kuingia mitini, kwa hiyo kwa kuwa hakuja hapa sitafanya kampeni maana imeshakwisha”.
Aliwataka wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi kumpigia kura Tyosera na pia kuhakikisha wanazilinda kura hizo.
Nape aliwataka Umoja wa Vijana wa CCM kuunganisha nguvu zao kuhakikisha siku ya uchaguzi kina mama na wazee wanakwenda kupiga kura bila kutishwa na yeyote hasa CHADEMA ambao alisema wana tabaia ya kukodi watu kutoka nje ya jimbo kuzuia wazee na wanawake kwenda kupiga kura.
Uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Urughu unafanyika kufuatia Tyosera ambaye alikuwa diwani wa CHADEMA kujiuzulu na kuhamia CCM, na baada ya kuhamia CCM amegombea katika kura za maoni na kuongoza kwa kura nyingi.
Akizungumza Tyosera alisema aliamua kuhama kujiuzulu na kuhamia CCM kwa sababu wakati akiwa diwani kwa tiketi ya CHADEMA kila akiwa katika baraza la Halmashauri alijiona kama kunguru ndani ya yangeyange.