ALIYEKUWA Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Mnauye leo ameonja joto la jiwe la Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam baada ya kumzuia kuzungumza na vyombo vya habari alipotaka kuzungumza yamoyoni baada ya kuvuliwa nafasi yake ya uwaziri.
Jeshi la Polisi lilizuia waandishi wa habari kuingia katika Hoteli ya Protea ya jijini Dar es Salaam sehemu ambayo Nape alitangaza kuzungumza na vyombo vya habari. Waandishi baada ya kuzuiwa walilazimika kubaki nje ya hoteli hiyo hadi alipotokea Nape ambaye naye alizuiwa kushuka kwenye gari na baadhi ya makachero wa jeshi la polisi.
Heka heka hizo na sukuma nikusukume zilifanikiwa kumrejesha nape ndani ya gari lake na baadaye kulazimika kuzungumza na vyombo vya habari akiwa ndani ya gari lake akiwa amesimama kwa juu, licha ya juhudia za makachero kumzuia asizungumze lakini alifanya hivyo.
Akizungumza kwa kifupi alimshukuru Rais John Magufuli kwa kumteuwa na amefanya kazi kwa uwezo wake wote na hadi alipoamua kuondolewa katika nafasi hiyo, aliwataka wanahabari kuendelea kumpa ushirikiano waziri aliyechukua nafasi yake, Dk. Harrison Mwakyembe kama walivyofanya kazi naye kabla ya kuondoka.
Alisema wakati akiunda kamati ya kuchunguza tuhuma za uvamizi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuvamia kituo cha Clouds FM alitarajia kupoteza baadhi ya mambo yaani kugharamika, hivyo kilichotokea ni suala ambalo anaamini lingemgharimu.
Alisema aliomba nafasi ya ubunge na baadaye aliaminiwa kuwa waziri hivyo anarudi kutumikia wananchi wake jimboni kama mbunge hivyo, kuwashukuru wote waliotoa ushirikiano akiwa katika nafasi hiyo.