Nape Ang’ara Mkutano Mkuu UVCCM Dodoma

Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akicharaza gita zito la besi na bendi ya Vijana Jazz, wakati wa Mkutano Mkuu wa nane wa UVCCM kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere mkoani Dodoma. (Picha na Bashir Nkoromo).

Wanachama wa umoja wa vijana kutoka nchi rafiki mbalimbali wakiwa kwenye mkutano huo (Picha na Ikulu).

Na Mwandishi Wetu

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi Nape Nnauye, amenogesha Mkutano Mkuu wa Nane wa Umoja wa Vijana wa CCM, UVCCM unaoendea mjini Dodoma. Licha ya viongozi wengi kushangiliwa wakati wa kuingia ukumbini, nderemo na shamaramshamra zililipuka zaidi kutoka kwa wajumbe wa Mkutano huo wakati Nape alipotangazwa kuwasili.

“Jembe, jembe, jembe”, wajumbe walisikika wakilipuka na kumshangilia baada ya Mkuu wa Umahasishaji na Chipukizi wa UVCCM, Esther Bulaya alipotangaza kuwasili kwa Nape ukumbini. Ukumbi ulilipuka zaidi Nape alipopanda jukwaani na kuliungurumisha gita zito la besi, wakati Bendi ya Vijana Jazz ilipokuwa ikitumbuiza wimbo maalum, baada ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuwasili ukumbini.

Shamra shamra zikihanikiza kwenye ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika mkutano wa nane wa UVCCM mjini Dodoma. (Picha na Ikulu)

Viongozi wengine walioonyesha kuwakuna wajumbe wa mkutano huo wa vijana ambao ni wa Uchaguzi Mkuu ni pamoja, na Mbunge wa Bumbuli Januari Makamba, Katibu wa NEC Uchumi na Fedha Mwigulu Nchemba na Katibu wa NEC Oganaizesheni, Asha Abdallah Juma.

Baada ya mkutano kufunguliwa na Rais Kikwete, uchaguzi uliendelea ambapo leo, wanatarajiwa kupatika viongozi wapya wa UVCCM ngazi ya Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Ujumbe wa Baraza Kuu UVCCM na wawakilishi kwenye jumuia zingine.

Katika nafasi ya Uwenyekiti ushindani ulihamia kwa wagombea wawili Msaraka Rashid Simai, Khamis Sadifa Juma baada ya mgombea mwingine Abdallah Lulu Mshamu kujitoa wakati wa kujieleza kwa wajumbe ukumbini. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti wamechuana Ally Salum Hapi, Paul Christian Makonda Mboni Mohamed Mhita wakati nafasi zingine ni, Halmashauri Kuu ya Taifa Viti sita (Bara) wagombea 40, Viti Vinne (Zanzibar) wagombea 22, Nafasi ya Baraza Kuu la Vijana Taifa Viti vitano Bara wagombea 39 na viti vitano Zanzibar wagombea 14, Uwakilishi Wazazi Taifa na Jumuia ya Wanawake Tanzania (UWT) wagombea 16 kila nafasi.