Nape amjibu Mpendazoe kuhusu waanzilishi wa CCJ

Na Edson Kamukara

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Itikadi na Uenezi, Nape Mnauye, ameendelea kukanusha madai ya kuhusika na uasisi wa Chama Cha Jamii (CCJ), akisema anayetaka kuwajua waasisi, aende kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.

“Iko Mamlaka ya kuelezea nani ni nani katika kila chama cha siasa hapa nchini na anayetaka kuwajua waasisi wa CCJ aende kwa John Tendwa, ataona kama Nape ni miongoni mwa waasisi kama inavyosemwa au la,” alisema Nape.

Mwanasiasa huyo aliyasema hayo jana Makao Makuu ya CCM Ofisi ndogo ya Limumba jijiji Dar es Salaam,wakati wa mkutano wake na waandaishi wa habari, akisema japokuwa waasisi wa vyama vyote vya upinzani wametoka CCM lakini yeye ni mwanachama hai asiyebabaika kuhama vyama.

“Siasa ni Itikadi, mimi siwezi kuhama CCM maana nimeridhika na itikadi hiyo, ndiyo maana niliwahi kusema kama yuko anayeweza kumsilimisha paka ajitokeze. Hizo taarifa zinazotolewa na Fred Mpendazoe ni za kuzusha,” alidai Nape.

Majibu ya Nape yanakuja ikiwa ni siku mbili toka kada wa CHADEMA, Mpendazoe kumtaja pamoja na vigogo wengine wa CCM kuwa walishiriki kuasisi CCJ lakini katika dakika za mwisho wakamsaliti Mpendazoe.

Wengine waliotajwa kwenye mpango huo wa uasisi wa CCJ ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa, Daniel Ole Porokwa na Paul Makonda.

Katika maelezo yake, Nape alisema kamwe hawezi kuhama vyama kama alivyofanya Mpendazoe kwa muda mfupi alipotoka CCM, akajiunga CCJ na kisha akahamia CHADEMA.

Kuhusu watuhumiwa wa ufisadi kupewa barua za kuwaondoa kwenye nyadhifa zao, Nape alisema hayo ni maamuzi ya chama ambayo lazima yatekelezwe, lakini akashuri kuwa ni vyema wale wanaotuhumiwa wakajiondoa mapema badala ya kungoja barua.

Kwenye mkutano wake huo, Nape alielezea mafanikio ya ziara ya Sekretariaeti ya NEC Taifa katika Mkoa wa Singida iliyofanyika Mei 10 hadi 15 mwaka huu, akisema chama kilivuna wanachama wapya 188 na 580 walijiengua kutoka CHADEMA.

“Changamoto kubwa iliyojitokeza kisiasa ni hali ya madiwani wa CCM kutojua vizuri wajibu wao na kusimamia rasilimali za umma zikiwemo fedha zinazopelekwa kwenye halmashauri toka Serikali kuu kusaidia maendeleo,” alisema Katibu huyo.

Aliongeza kuwa wameridhishwa na utekelejazi wa Ilani ya Uchaguzi katika kufanikisha miradi ya ujenzi wa Hospital mpya ya rufaa ya Mkoa wa Singida, mradi wa uboreshaji huduma za maji safi na salama Singida Mjini na ile ya barabara.