Nape Aishutumu CHADEMA Kupanga Uhalifu

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi Nape Nnauye

Na Mwandishi Wetu, Moshi

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi Nape Nnauye amesema ipo haja ya kuangalia upya sheria ya vyama vya siasa nchini kama ina meno ya kutosha kudhibiti vyama vinavyojigeuza kutoka vyama vya siasa kuwa vyama vinavyopanga na kuratibu uhalifu na ugaidi nchini.

“Hivi sheria ya vyama vya siasa inasemaje juu ya vyama vinavyojigeuza kwa makusudi kutoka vyama vya siasa na kuanza kuwa vya kupanga na kuratibu machafuko, utekaji, uhalifu na dalili za ugaidi? Kama sheria zilizopo hazitoshelezi zitazamwe upya ili tusije iingiza nchi kwenye machafuko kwa kisingizio cha vyama vingi”, alisema Nape.

Nape alisema huku akionekana wazi kurusha makombora hayo kwa viongozi wa Chadema, akidai baadhi ya matukio ya kihalifu ambayo yamekuwa yakitokea nchini yamekuwa yakipangwa na kuratibiwa na viongozi wa chama hicho kutimiza ahadi yao ya kuhakikisha nchi haitawaliki.

“Hivi watu wanaanza kutangaza hadharani kuwa watahakikisha nchi haitawalikiu, wakaanza kugomea baadhi ya shughuli za serikali na wanapoona hailipi sasa wanaanza kupanga, kuratibu na kusimamia utekelezaji wa uhalifu, machafuko na sasa iko dalili dalili za vitendo vya kigaidi, bado tunawaita chama cha siasa?”, alihoji Nape.

Nape alisema anashangazwa na jinsi viongozi wa Chadema wanavyotapatapa na sakata linalokabili baadhi ya viongozi wao wa ngazi za juu kuhusishwa na vitendo vya kigaidi, na kwamba kinachowasumbua sasa ni dhambi ambayo anadai chama hicho kimeipanda chenyewe kwa muda mrefu.

“Rafiki zangu hawa wamepanda mbegu chafu kwa muda mrefu. Wenzetu waliamua kujenga Chama kwa msingi wa chuki na uongo, sasa walisahau mwisho wa chuki aibu mchimba kisima huingia mwenyewe”, alisema Nape.

Nape alidai anasikitika kwa nini Chadema kimeamua kujimaliza, kwa kijijenga katika misingi ya kujigengea umaarufu kwa kusema uongo na chuki na mafarakano vitu ambavyo sasa vinaanza kuwaumbua kwa kuwa njia ya mwongo ni fupi na mshahara wa dhambi ya uongo ni mauti.

Alisema CCM kimeendelea kuwa Chama bora kwa sababu kilijengwa tangu awali katika misingi ya haki na kujali wananchi na kuweka bayana misingi yake ya uongozi. “Ndiyo sababu hadi sasa kinaendelea kutawala, lakini ni kwa sababu ukiona vinaelea vimeundwa”, alisema Nape.

Nape alisema, baada ya CCM kufanya kazi ya ukombozi na kuwaunganisha Watanzania na kuwa kitu kimoja, sasa kinafanyakazi ya kuboresha maisha ya Watanzania kwa kuwa kazi hiyo ya ukombozi na kuunganisha watu ilikwisha kamilika kwa ufasaha mkubwa.

Alisema, lisema katika jitihada zake za kuwaletea wananchi maendeleo, imehakikisha kila eneo la Tanzania linawekwa kwenye mipango ya maendeleo ukiwemo mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro.

“Hawa Chadema wanawadanganya Moshi, eti kwa kuwa wao ndiyo wenye Halmashauri kwa hivyo wao ndiyo wameleta maendeleo. Huu ni ungo mkubwa”, alisema, Nape nakubainisha kwamba mipango yote ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Moshi, ni utekeleza wa ilani ya CCM kwa sababu mipango yote ipo na imeandikwa katika ilani ya chama hicho.

Akizungumzia Chadema, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA), Juliana Shonza aliwataka Watanzania kuacha kuwaunga mkono Chadema katika mipango yao ya maandamano ya mara kwa mara ambayo yanavuruga nchi.

“Vijana jihadharini sana na hawa Chadema, msipumbazike na kugeuzwa asusa zao, maana wao huandaa maandamano ili wawapige picha kisha picha hizo huzipeleka kwa wafadhili wao kwa ajili ya kujipatia fedha, je na ninyi fedha hizo huwa mnapewa?”, alihoji Shonza.

Akianza kuhutubia, Nape aliwaomba wananchi kusimama kwa dakika moja kuwaombea na kuwakumbuka wale wote walioathiriwa na matendo mbalimbali aliyodai hufanywa na Chadema, hatua iliyofuatiwa na mamia kwenye mkutano huo kusimama kwa dakika moja na kisha kusema amina kabla ya kuketi chini.

“Kwani uongo? kwani wewe hujatambua kwamba Chadema wamekuwa wanapanga na kuratibu matendo ya kihalifu na kigaidi, kwa kweli ni heri tukawakumbuka na kuwaombea walioathirika na vitendo vya chama hiki”, alisema, Juma Shangali mkazi wa Kiboriloni, Moshi.

Katika mkutano huo, vijana 65, wakiongozwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema wa wanafunzoi wa vyuo Vikuu, Juma Ramadhani anayesoma Chuo Kikuu cha Ardhi walirejea CCM na kuabidhi kadi zao za Chadema kwa Nape.