*Nakala zaidi ya 650,000 kusambazwa kwenye taasisi
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema hadi kufikia Februari 26, mwaka huu, Serikali imekwishasambaza jumla ya nakala 1,341,300 za Katiba Inayopendekezwa Kwenye mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Machi 11, 2015 Waziri Mkuu alisema Zanzibar imepatiwa nakala 200,000 na kuongeza kuwa nia ya Serikali ya kuchapisha nakala milioni mbili iko palepale.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alibainisha kwamba nakala 658,700 zilizobakia zitagawanywa Kwenye wizara zote za Tanzania Bara na Zanzibar, Mahakama, Bunge, Baraza la Wawakilishi, taasisi za Serikali, Tume zote, taasisi za dini, asasi za kiraia, vyombo vya sheria, vyuo vya elimu ya juu, vyama vya siasa na na taasisi zinazojitegemea ili kuongeza wigo wa usambazaji kwa wananchi wengi zaidi.
“Lazima nikiri kwamba kuzisambaza na kuzifikisha kwa walengwa ni jambo moja na kuhakikisha kwamba zinasomwa ni jambo jingine. Wito wangu kwa Watanzania wote ni kuhakikisha wanasoma na kuielewa Katiba Inayopendekezwa ili wanapokuja kupiga kura waelewe ni nini wanafanya,” alisema.
“Niwasihi sana Watanzania wenzangu, wasikubali kurubuniwa juu ya kilichoandikwa Kwenye Katiba Inayopendekezwa, na tena mtu asikubali kuombwa kuomba auze nakala yake. Tusikubali watu warubiniwe kirahisi. Kila mmoja ahakikishe anaisoma na kuielewa, na wenye mitandao na blogs watumie fursa hii kuusambazia umma nakala za Katiba hii ili watu wengi zaidi waweze kuisoma,” alifafanua.