NAIBU Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amemtaka mkandarasi China Civil Engeneer Construction Cooporation (CCECC), anayejenga barabara ya Mafinga-Nyigo km 74.1 na (CRSG) anayejenga sehemu ya Nyigo –Igawa KM 63.8 kuongeza kasi ya ujenzi ili upanuzi na uimarishaji wa barabara hiyo ukamilike kwa wakati.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi huo Eng. Ngonyani amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Iringa Eng. Daniel Kindole kuhakikisha upana wa barabara hiyo na ubora wake unakidhi malengo ya Serikali ili barabara hiyo ili idumu kwa muda mrefu na kupunguza msongamano na ajali zinazoepukika.
“Barabara hii ambayo ni sehemu ya barabara kuu ya TANZAM inaunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi za Zambia na Malawi ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi hivyo ni lazima isimamiwe kikamilifu ili idumu kwa muda mrefu”, amesisitiza Eng. Ngonyani.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa Eng. Daniel Kindole amesema tayari kilomita 18 kati ya 74.1 katika sehemu ya kwanza ya Mafinga –Nyigo imeshawekwa lami na Mkandarasi ameunda timu tatu ili kuharakisha ujenzi huo.
“Ujenzi wa barabara ya Mafinga -Igawa unahusisha mikoa mitatu ambapo Kilomita 74.1 ziko katika mkoa wa Iringa Mafinga-Nyigo, Kilomita 52 ziko katika mkoa wa Njombe Nyigo-Halali na Kilomita 12 ziko katika Mkoa wa Mbeya Halali-Igawa hivyo mimi pamoja na wenzangu tumejipanga kuhakikisha barabara hii inakamilika Novemba mwakani kama ilivyopangwa”, amesisitiza Eng. Kindole.
Naye Meneja Mradi wa ujenzi wa barabara hiyo Sehemu ya Mafinga – Nyigo KM 74.1 Richard Guo amemhakikishia Naibu Waziri huyo kwamba kasi yao ya ujenzi ni nzuri na barabara hiyo imeimarishwa ili kukidhi mahitaji na itakamilika kwa wakati. Zaidi ya shilingi bilioni 116 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya kwanza yaani Mafinga- Nyigo km 74.1 ambazo zinagharamiwa na Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.