Naibu Waziri Kazi, Vijana na Ajira, Atembelea Kambi Tiba ya GSM Dodoma

Mavunde akisikiliza maelezo ya mmoja kati ya wagonjwa waliohudhuria kambi tiba ya GSM.

Mavunde akisikiliza maelezo ya mmoja kati ya wagonjwa waliohudhuria kambi tiba ya GSM.

Na Mwandishi Wetu
Mbunge wa Dodoma Mjini na Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde amefanya ziara ya kushtukiza katika kambi tiba ya GSM Foundation inayofanywa na kikosi cha Madaktari bingwa kutoka hospitali ya MOI, ambayo kuanzia imepiga kambi Dodoma baada ya kutoka katika mikoa ya Mwanza, Singida, na Shinyanga.

Akieleza sababu za kuitembelea kambi hiyo ambayo iko katika hatua zake za mwisho kumaliza awamu ya kwanza, Mavunde amebainisha kwamba kwanza, ni kwa sababu alisikia kambi iko katika jimbo lake, lakini jingine kubwa na la msingi likawa ni kupeleka shukrani zake kwa Maafisa wa Taasisi ya GSM wanaoambatana na madaktari kuweka kambi tiba hizo katika kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa na vichwa vikubwa na migongo wazi kila mwaka.

Mavunde akiongea na wanahabari waliokuwa hospitalini hapo kufuatilia habari za wagonjwa waliohudhuria kambi tiba ya GSM.

Mavunde akiongea na wanahabari waliokuwa hospitalini hapo kufuatilia habari za wagonjwa waliohudhuria kambi tiba ya GSM.

“Nimeshtushwa na takwimu za mwaka juzi, kwamba wanaozaliwa ni 4000 na wanaorudi hospitali kwa ajili ya tiba hawazidi 600. Hii ni hatari, ilipaswa mtu kuchukua jukumu la haraka na nimeshukuru kusikia GSM mmefanya hilo, hongereni sana”, alisema Mavunde.

Mavunde amewataja Maafisa wa GSM na Madaktari kuwa ni watu wenye moyo wa kizalendo ambao wanatakiwa kuigwa na jamii, wameacha familia zao, na wameamua kuokoa maisha ya watoto ambao hata hawawajui, kwa sababu moja tu kubwa na ya msingi ya utanzania.