Naibu Waziri Injinia Ngonyani Aridhishwa na Kasi ya Utendaji wa TBA

Muonekano wa baadhi ya Nyumba zinazojengwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA) Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam zikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake.

NAIBU Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani ameupongeza Wakala wa Majengo Nchini (TBA), kwa jitihada wanazozifanya katika kuongeza mapato na kununua vifaa vipya na kisasa vitakavyowezesha wakala huo kumudu ujenzi wa miradi mingi mikubwa kwa wakati.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa nyumba 851 ulioko Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Eng. Ngonyani ameeleza kuridhishwa kwake na mabadiliko makubwa ya utendaji yanayoendelea katika wakala huo.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba za kisasa za makazi ya watu, ongezeni ubunifu ili nyumba zote zinunuliwe na kuwawezesha Watanzania kupata makazi bora kwa bei nafuu,” amesema Eng. Ngonyani.

Ameitaka TBA kuhakikisha inapata faida ili kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali kama ilivyo kwa taasisi nyingine za Umma na hivyo kuiwezesha Serikali kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Ongezeni kasi katika ukusanyaji wa madeni kwa watu binafsi wanaokaa kwenye nyumba zenu na sisi Wizarani tutawasaidia katika kuhakikisha mnalipwa kwa wakati kwa wadaiwa wa Serikalini” amesisitiza Eng. Ngonyani.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya TBA katika ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo yanatarajiwa kukabidhiwa kwa chuo hicho wiki ijayo.

Mbweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,840 yamejengwa na TBA katika kipindi kisichozidi miezi sita na yamegharimu takribani shilingi bilioni 10. Naye Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Elius Mwakalinga amemhakikishia Naibu Waziri Eng. Ngonyani kuwa Wakala huo umejiimarisha kwa kuwa na vifaa vya kisasa na watendaji wenye sifa hivyo Serikali iendelee kuuamini na kuupa miradi mingi ya ujenzi wa nyumba na ofisi.

“Tunao wahandisi 74, wachoraji ramani 66, wakadiriaji majenzi 52 na bado tunao wataalam mbalimbali kutoka kwenye vyuo vikuu nchini wanaowezesha wakala wetu kuwa imara wakati wote’ amesema Arch. Mwakalinga.

Naibu Waziri Eng. Ngonyani yuko katika ziara ya siku mbili ya kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi inayosimamiwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA) jijini Dar es Salaam.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikali, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano