Naibu Waziri Fedha Atolea Ufafanuzi Mgogoro wa EFD

Naibu Waziri wa Fedha  Saada Mkuya  Salum (kulia)akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu utata wa vifaa vya kieletronik vya kutoa risiti (EFD)

Naibu Waziri wa Fedha  Saada Mkuya  Salum (kulia)akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu utata wa vifaa vya kieletronik vya kutoa risiti (EFD)


Na Magreth Kinabo

SERIKALI imesema imeshaelekeza wasambazaji wa vifaa vya eletroniki vya kutoa risiti (EFD) kuuzwa  kwa bei tofauti kulingana na ubora wa vifaa hivyo kwa mtumiaji.

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salum wakati akizungumza na waandishi wa habari leo kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu J. K. Nyerere jijini Dar es Salaam kutolea ufafanuzi suala hilo.

Naibu Waziri huyo, alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali na waandishi wa habari kufutia mgomo wa wafanyabiashara unaoendelea katika baadhi ya mikoa kufutia kifaa hicho kuuzwa kwa bei ya Sh. 700,000 hadi 800,000 ambayo wengi wa wafanyabiashara wanadai ni ghali sana.

“Utumiaji wa EFD si kumkomoa mfanyabiashara bali ni kuongeza mapato ya Serikali katika kuendeleza maendeleo ya nchi”.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo alisema vifaa hivyo vipo vinavyouzwa kuanzia bei ya 100,000 na kuendelea, hivyo na kuwataka wasambazaji kuuza vifaa hivyo kulingana na bei iliyopangwa huku wakizingatia ubora na matumizi anuai ya kifaa hicho.

Wafanyabiashara mikoa kadhaa sasa wamekuwa wakijitokeza kugomea kuvinunua vifaa hivyo wakidai vinauzwa ghali mno huku wengine wakidai ni miradi ya baadhi wa vigogo ambao ndio wanaoshinikiza pasipo wafanyabiashara kuhusishwa katika mchakato wake kikamilifu.

WAKATI HUO HUO; Serikali imesema kwamba itaendelea kuelekeza rasilimali katika masuala ya elimu, afya, kilimo ikiwa ni hatua ya kuweza kupunguza umasikini kwa haraka ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto zilizopo katika sekta mbalimbali .

 Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Waziri wa Fedha  Saada Mkuya  Salum wakati akizungumza na waandishi wa habari leo kuhusu mkutano wa mwaka. 2013 wa kupitia  utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali (GBS) ulioshirikisha na Washirika wa Maendeleo(DPs) na wadau mbalimbali kutoka serikalini uliofanyika kwenye ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu J.K. Nyerere jijini Dares Salaam.

 “Changamoto inayotukabili ni kuleta maendeleo kwa haraka. Uchumi wa nchi unakuwa kwa asilimia 7 lakini umasikini umepungua kwa asilimia 2,”alisema Waziri huyo.

 Alisema  changamoto inayoikabili serikali ili kukabiliana na umasikini nchini ni kuhakikisha inaelekeza rasilimali zake  ili ziweze kuzalisha ajira .Pia  kuangalia idadi ya watu  kulingana na uchumi wa nchi.

 Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri huyo kufuatia Mwenyekiti wa Washirika wa Maendeleo Balozi wa Sweden, Lennarth  Hjeimaker kueleza  kuwa hatua za kupunguza umasikini na upatikanaji wa huduma za jamii bado ni ndogo, kiwango cha ufaulu kwa shule za sekondari na msingi kushuka na uwiano wa walimu na wanafunzi bado mdogo, zaidi ya nusu ya watu vijijini  wahapati maji safi na salama na upatikanaji wa nishati vijijini bado ni changamoto.

 Wadau hao pia wameishauri Serikali kuendelea kupambana na tatizo la rushwa nchini.
 Katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita 2012/2013 wadau hao walichangia Dola za Marekani milioni 560 na mwaka huu wa fedha waliahidi kutoa Dola za Marekani milioni 561 hivyo hadi sasa Serikali imeshapokea Dola za Marekani milioni 290.2.