Na Janeth Mushi, Arusha
MAOFISA ugani na kilimo nchini wametakiwa kuhama maeneo ya mjini na kwenda vijijini ili kuwasaidia wakulima na wafugaji mbinu anuai za kilimo cha kisasa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika sekta hiyo muhimu hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa katika kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya wakulima na wafugaji, Nane Nane juzi na Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Agrey Mwandri, alipokuwa akizungumza katika sherehe hizo.
Mwandri alisema ili kufanikisha hilo wakuu wa mikoa, wilaya kwa kushirikiana na wakuregenzi wa halmashauri hawana budi kuhakikisha maofisa ugani wanawafikia wakulima ambao wengi wao wanaishi maeneo ya vijijini.
Naibu Waziri huyo alisema wakulima wengi wao wanaishi vijijini na wamekuwa wakilima kilimo cha mazoea badala ya kulima kilimo cha kisasa na chenye tija kutokana na kukosa elimu ya kutosha kutoka kwa wataalamu ambao siku zote wanajichimbia mjini.
“Maofisa ugani na maofisa kilimo ondokeni wilayani na mijini, nendeni vijijini mkawafundishe wakulima mbinu za kilimo cha kisasa ili waweze kuongeza uzalishaji na kuboresha mazao yao,” alisema Mwandri
Aidha Mwandri aliwataka wakulima kuimarisha kilimo kwa kutumia mbinu za kiteknolojia ili waweze kusonga mbele na kuweza kupata mafanikio kupitia sekta hiyo ya kilimo na ufugaji ambayo watu wengi wamekuwa na dhana potofu, kuwa haiwezi kuwaletea maendeleo jambo ambalo si la kweli.
“Tukilima kilimo kisichokuwa na tija hatutawezakusonga mbele, na kupitia maonesho haya nina imani mtakuwa mmejifunza mbinu za kilimo cha kisasa ili mnapotoka hapa muende keendeleza kilimo cha kisasa na chenye tija kwenu,” alisema Naibu Waziri huyo.
Hata hivyo aliwataka wakulima na wafugaji kujiunga na vyama vya Ushirika (SACCOS) ili kupitia ushirika huo waweze kupatiwa mikopo na benki na taasisi za fedha.
“Ushirika ndiyo silaha pekee ya wanyonge ambayo itaweza kuwasaidia na kuweza kujiinua kiuchumi, hivyo naagiza maafisa ushirika kuwapatia wakulima elimu juu ya umuhimu wa kujiunga na vyama hivyo ili kuweza kujiinua kiuchumi,” alisisitiza Mwandri
Akizungumzia suala la mogogoro baina ya wakulima na wafugaji inayotokea katika maeneo mengi hapa nchini, Mwandri alizitaka halmashauri za Wilaya kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi sambamba na kutoa elimu kwa wananchi.