Baadhi ya Viongozi na watendaji wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na wawekezaji wakifuatilia mazungumzo hayo leo 10/10/2016 Jijini Dar es Salaam. |
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Anastazia Wambura amekutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji wa makampuni matatu kutoka China, lengo la ziara la wawekezaji hao likiwa ni kufanya utafiti kujua ni namna gani Kampuni ya StarTimes inapiga hatua katika kusaidia kukuza maendeleo katika sekta ya habari Tanzania.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Wizarani hapo, Mhe. Wambura amesema kuwa Serikali iko mbioni kujenga Jengo Maalum kwa ajili ya shughuli za Kiutamaduni (Cultural Complex) ambalo linatarajiwa kujengwa Bagamoyo na ndani ya jengo hilo kutawekwa vitu mbalimbali vinavyohusu utamaduni wa Tanzania.
Ameeleza kuwa, Tanzania imekuwa ikishirikiana na China katika masuala mbalimbali yakiwemo ya michezo, utamaduni na Sanaa ambapo baadhi wa wageni kutoka China wamekuwa wakifika kutalii na kuwekeza, lakini pia baadhi ya Watanzania nao wamekuwa wakipata fursa ya kutembelea China kujionea maendeleo na kujifunza mambo mbalimbali.
“Tanzania inapenda kushirikiana na China katika mambo mbalimbali kama vile kutengeneza filamu, michezo na hata utamaduni, kwakweli ushirikiano huu umekuwa wa manufaa kwetu sisi Watanzania kwani unapanua wigo wa kukuza maendeleo”, alisema Mhe. Wambura.
Ameongeza kuwa, Kampuni ya StarTimes ni moja kati ya Makampuni yaliyoisaidia Tanzania kuhama toka Analojia kwenda Dijitali ambapo kampuni hiyo iliweza kuwekeza nchini kwa kuleta ving’amuzi vyenye bei nafuu kiasi cha kumwezesha Mtanzania wa hali ya chini kumudu kununua na kuweza kupata habari kupitia runinga yake.
Aidha, amewashauri wawekezaji hao kutengeneza makala mbalimbali zinazohusu utamaduni wa Kitanzania kwa kushirikiana na Watanzania kwani inaweza kuleta soko zuri ndani na nje ya nchi. Kwa upande wake Kiongozi wa msafara wa wawekezaji hao ambaye pia ni Afisa Mkuu wa Kampuni ya Star Media (T) Ltd Bw. Leo amesema kuwa, China itaendeleza ushirikiano na Tanzania ambapo iko mbioni kutoa nafasi kwa Watanzania kutoka Shirika la Utangazaji TBC na Wizara kwenda kujifunza namna ya kutengeneza habari ikiwemo Makala na upigaji picha ili taaluma hiyo ije kuwasadia wengine.
Mbali na kuja kutafiti namna Kampuni ya StarTimes inavyofanya vizuri katika kuleta maendeleo Tanzania, ujio wa wawekezaji hao nchini pia unafungua milango zaidi ya kibiashara baina ya Tanzania na China na kuendeleza ushirikiano wenye lengo la kuleta maendeleo.