NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dk. Hamisi Kigwangalla leo amelazimika kusimama getini baada ya muda wa kuingia kazini asubuhi (saa 1:30) kufikia kikomo huku akiamuru walinzi wafunge geti na waliochelewa kujieleza kwa barua.
Amesema zoezi hilo limefanyika ili kuhakikisha wafanyakazi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee kuzingatia suala la muda wa kufanyakazi kuanzia kuingia kazini hadi muda wa kutoka kama ulivyopangwa. Dk. Hamisi Kigwangalla alikuwa akifuatilia suala la nidhamu ya kujali muda wa kuwahi kazini kwa watumishi wa wizara hiyo leo jijini Dar es salaam.
“Wafanyakazi wanawajibu wa kuwahi kazini saa 1:30 asubuhi kama ilivyopangwa kwa mujibu wa taratibu za utumishi wa umma na kutoka saa 9:30 baada ya muda wa kazi, hatuwezi kuendelea kuvumilia tabia ya watu kuendelea kumwibia mwajiri muda wa kufanyakazi”,
“Sisi tumewahi kazini, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na vionozi wengine, halafu watumishi wanachelewa, tumeonesha mfano, tunawahi na tunachelewa kuondoka,” alisema Dk. Kigwangalla.
Kwa mujibu wa taratibu za kazi, ilipofika saa 1:30 asubuhi, Dk. Kigwangalla aliamuru walinzi kufunga geti na kutoruhusu waliochelewa kuingia hadi atakapo maliza kusaini madaftari ya mahudhurio kulingana na idara na vitengo vilivyopo wizarani hapo.
Idara hizo ni pamoja na Utawala, Kinga, Mafunzo, Tiba, Udhibiti na Uhakiki Ubora, Mganga Mkuu, Uhasibu, Sera na Mipango, Wauguzi na Famasia pamoja na vitengo vya Sheria, Mawasiliano Serikalini na Tehama.
Akisisitiza Dk. Kigwangalla alisema kuwa wanachokifanya ni kuhakikisha zoezi la kukomesha tabia ya uchelewaji linakuwa endelevu kwasababu watumishi wameajiriwa ili kuwahudumia wananchi, ufuatiliaji huo utakomesha tabia ya watumishi kuchelewa kufika kazini na kuondoka mapema kabla ya muda wakazi.
Vilevile Dk. Kigwangalla alisema kuwa watumishi wafanye kazi kwa kujitolea, maana Tanzania itajengwa na zama za kazi ambapo wao viongozi wamewapa watumishi mfano wa kuwahi kazini.
Kuhusu watumishi waliochelewa Dk. Kigwangalla ameagiza waandike barua za kujieleza ni kwake na azipate leo ambapo zoezi hilo la amemkabidhi Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bw. Michael John. Aidha, katika kudhibiti tabia ya uchelewaji, Dk. Kigwangalla amemwagiza Bw. Michael amueleze kwa maadishi ni kwanini Wizara hiyo haijachukua hatua ya kuingia katika mfumo wa dijiti (Biometric) wa watumishi kuweka vidole au kutumia kadi wakati wa kuingia kazini ili mfumo mzima wa ofisi ujue mtumishi fulani amefika kazini saa ngapi na kama atatoka ajulikane yupo wapi na kwa nini.
Dk. Kigwangalla amesema kuwa amefikia hatua hiyo ya kusimamia kukomesha tabia ya uchelewaji kutokana na Wizara hiyo kulaumiwa kwa urasimu, kumbe watumishi hawawahi kazini ambapo yeye mwenyewe amejionea nia watu wangapi wamewahi kazini. Zaidi ya hayo, Dk. Kigwangalla ameagiza kupewa maelezo ya kina juu ya watumishi wa afya nchi nzima kuanzia Madaktari, Wauguzi, Wafamasia ili aweze kujua kuna mfumo gani wa kuangalia watumishi wamefika ofisini na wanafanya kazi ipasavyo.