Na Mwandishi Wetu
NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amewashangaa na kuwabeza wanaokejeli Serikali ya Awamu ya Nne ya Uongozi wa Tanzania, chini ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kuwa haijafanya lolote kuwaletea wananchi maendeleo.
Amesema kuwa yeye binafsi ameshuhudia mazuri mengi na mafanikio mengi yaliyoongozwa na Serikali ya Rais Kikwete kwa kuanzia kwenye eneo lake mwenyewe.
Naibu Spika Ndugai ameyasema hayo Aprili 11, 2013 wakati alipopewa nafasi ya kuwasilimia wananchi kwenye Sherehe ya Uzinduzi wa Mradi wa Ukarabati na Upanuzi wa Miundombinu ya Kusambaza Umeme Mkoani Dodoma na Wilaya ya Kiteto, Mkoa jirani wa Manyara chini ya Ufadhili wa Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Millenium Challenge Corporation (MCC).
MCC imetoa kiasi cha Sh. Bilioni 28.5 (sawa na dola 17.8) kwa ajili ya ujenzi wa Mradi huo wa Kusambaza Umeme ikiwa ni sehemu ya msaada wa dola za Marekani milioni 698 (sawa na Sh. trilioni 1.19) wa ujenzi wa miradi mingi ya miundombinu katika Tanzania.
“Mheshimiwa Rais, nianzie kwenye kijiji cha Mkoka ambako tulipo kwa sasa na nieleze nini Serikali yako inakifanya kijiji hiki katika mwaka huu wa Bajeti ili kuthibitisha jinsi Serikali yako chini ya uongozi wako inavyochapa kazi,” amesema Naibu Spika Ndugai na kuongeza:
“Serikali yako imekipa kijiji cha Mkoka sh. milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa soko la kisasa na ujenzi huo unaendelea. Tunajenga machinjio ya kisasa kwa gharama ya sh. milioni 40. Tunajenga mradi mkubwa wa maji kwa kiasi cha sh. milioni 600 na shule zetu mbili tayari zimejengewa madarasa ya nyongeza katika mwaka huu wa fedha,” amesema Ndugai na kuzidi kumwambia Rais Kikwete:
“Siyo hivyo tu. Serikali yako Mheshimiwa Rais imetuwezesha kupata fedha na raslimali nyingine za kujenga ghala la mazao, kujenga maabara mpya kwenye Sekondari yetu ya Kata na tumepatiwa kiasi cha sh. milioni 700 kwa ajili ya ujenzi wa barabara mbili ambazo zote zitaishia kwenye Soko la Kimataifa la Mahindi la Kibaigwa, ujenzi ambao utawezesha wakulima kufikisha mahindi yao kwenye soko hilo kwa urahisi kuliko ilivyo sasa.”