IKIWA ni siku chache baada ya madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kumaliza tofauti zao kisiasa na Chama Cha Mapinduzia (CCM) katika Manispaa ya Arusha, Naibu Meya wa manispaa hiyo, Estomihi Malla kutoka CHADEMA jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kutimuliwa na mlinzi wa Shule ya Sombetini akiwa katika ukaguzi wa shule zilizopata fedha kutoka Mfuko wa TASAF.
Naibu Meya huyo akiwa katika ziara ya Kamati ya Fedha ya Manispaa ya Arusha, alikumbana na sakata hilo baada ya kuingia katika geti la shule hiyo akiwa na madiwani wenzake, ambapo mlinzi wa shule hiyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja kumtaka Malla na kamati yake kutoka nje ya geti kwa madai kuwa hana taarifa zozote kutoka kwa mkuu wa shule hiyo juu ya ujio wao.
“Naomba mtoke nje ya geti mara moja, sina taarifa kutoka kwa mwajiri wangu, naomba mtoke nje, sihitaji kuzungumza na yoyote wala siruhusu kuendelea kuwemo hapa ndani,” alisema mlinzi huyo kwa ukali.
Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa tisa mchana wakati Naibu Meya huyo akiwa katika ziara maalumu kutembelea ujenzi wa miradi mbalimbali ya manispaa hiyo inayotekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Jamii (TASAF) awamu ya pili.
Baada ya kamati hiyo kugoma kutoka ndani ya eneo la shule hiyo, mlinzi huyo aliingia ndani ya moja ya ofisi za shule hiyo na kutoka na upinde na mishale zaidi ya 30 inayosadikiwa kuwa na sumu.
Kufuatia hali hiyo Diwani wa Kata ya Elerai John Bayo ambaye pia ni mwenyekiti wa madiwani wa CHADEMA Wilaya ya Arusha, aliwasihi wajumbe wa kamati hiyo kutoka nje huku akisema kuwa watamshitaki mlinzi huyo kwa wakuu wake wa kazi.
Mara baada ya kutoka nje ya eneo la shule hiyo Meya wa Manispaa ya Arusha Gaudance Lyimo (CCM) ambaye pia alikuwa katika ziara hiyo, aliisihi kamati hiyo kuacha kukagua mradi huo na kuelekea katika kata ya Sokon I huku akisema kuwa watamuwajibisha mkuu wa shule hiyo kwa kuajiri mlinzi ambaye anakiuka maadili ya kazi ya Ulinzi.
“Hatuwezi kuwa na walinzi wa namna hii katika shule zetu nawasihi tuingie kwenye magari tuendelee na ziara kwenye kata nyingine na tutamuwajibisha mkuu wa shule hii,” alisema Lyimo. Akizungumza kwa njia ya simu mwenyekiti wa Kamati ya mradi (TASAF) katika shule hiyo Gerald Munisi, alidai kuwa hakuwa na taarifa zozote juu ya ziara ya viongozi hao wa Manispaao kukagua mradi shuleni hapo.
Wengine waliotimuliwa na mlinzi huyo ni Alphonce Mawazo diwani wa Sombetini(CCM), Ismail Katamboi (CCM) kata ya Olasiti, Mary Kisaka diwani viti maalumu (CCM), Michael Kivuyo(TLP) kata ya Sokon I na Reuben Ngowi (CHADEMA).
Katika ziara hiyo awali madiwani hao walitembelea shule za Sekondari Elerai, Shule ya Msingi Muungano na Shule ya Msingi Levolosi napo kukagua miradi inayofadhiliwa na fedha kutoka katika mradi wa TASAF.