Nahodha: Sijui DCI Manumba alikoitoa ripoti ya Mwakyembe

Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha

*Asems uchunguzi unaendelea na matokeo atayatangaza yeye, ataka Manumba aulizwe mwenyewe chanzo cha taarifa

WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha amesema uchunguzi kuhusiana afya ya Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe bado unaendelea na ni yeye atakayetangaza matokeo ya kama alipewa sumu au la baada ya kukamilika huku akiikana ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) Kamishna, Robert Manumba.

Hii ni mara ya kwanza kwa Nahodha kutoa tamko hilo tangu kuibuka kwa mjadala kuhusu afya ya Dk Mwakyembe hasa baada ya DCI Manumba kuutangazia umma kwamba ripoti kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaonyesha kuwa Naibu Waziri huyo hakulishwa sumu, kauli ambayo ilipingwa na Waziri mwenye dhamana ya Afya, Dk Haji Mponda na Dk Mwakyembe mwenyewe.

Akizungumza katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar es Salaam jana, Nahodha alisema uchunguzi kuhusu afya ya Dk Mwakyembe ni wa kisayansi na hauwezi kufanyika ndani ya wiki mbili au mwezi.

“Ninachosema ni kwamba uchunguzi nilioutangaza bado unaendelea,” alisema na kuongeza: Sasa mimi nimetangaza matokeo ya uchunguzi? Mimi ndiyo Waziri nasema uchunguzi bado unaendelea na mimi ndiyo nitatangaza hitimisho la jambo hilo.”

Alisema suala la Dk Mwakyembe ni zito na siyo la mtu kukurupuka kwani linagusa hisia za watu na kutahadharisha baadhi ya watu wanaojaribu kulifanya jepesi wanachezea kitu hatari.

“Ndiyo maana nasema ni jambo linalohitaji weledi wa hali ya juu katika kulichunguza. Ni jambo zito la kisayansi, naomba nipewe muda ili uchunguzi nilioagiza ufanyike kwa kina. Nasisitiza ni jambo linalohitaji weledi wa kisayansi.”

Waziri Nahodha alisema uchunguzi huo unafanyika kwa kuhusisha jopo la wataalamu wa sayansi hivyo kuwataka Watanzania kutambua kwamba uchunguzi huo unaendelea na ni vigumu kutamka utakamilika lini.

Kuhusu ripoti ya DCI

Alipoulizwa ni kwa nini asimchukulie DCI Manumba hatua kwa kutoa tamko wakati uchunguzi alioagiza haujakamilika alisema: “Ndiyo maana nasema, uchunguzi wa suala hili unaendelea. Sasa hatima yote hayo unayozungumza nasema nipeni muda.”

Alipoulizwa ni wapi DCI Manumba alipata ripoti ya Dk Mwakyembe wakati mgonjwa mwenyewe na Waziri wa Afya wameikana, alijibu: “Sasa, hilo ni vyema ukamtafuta yeye mwenyewe DCI aseme. Mtafute aseme yeye na Waziri wa Afya, hao watu wawili wanaweza kuzungumzia ripoti hiyo, lakini mimi nasema uchunguzi wa jambo hili la Dk Mwakyembe ni wa kisayansi na bado unaendelea.”

CHANZO: Mwananchi, kusoma habari hii zaidi tembelea:- www.mwananchi.co.tz