Na Said Mwishehe
Dodoma
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha amesema kubomolewa kwa mabanda 73 ya wafanyabiashara mjini Unguja Zanzibar ni uvunjifu wa sheria hivyo atahakikisha sheria kali zinachukua dhidi ya watakaohusika.
Nahodha amesema haamini kama tukio hilo lina uhusiano na mambo ya kisiasa ama ubaguzi, hivyo kuomba viachiwe vyombo vya sheria ili viweze kutekeleza majukumu yake.
Mwishoni mwa wiki katika eneo la Mchangani na Kiwengwa Unguja Kaskazini kumetokeoa tukio la kuchomwa kwa mabanda 73 ya wafanyabiashara jambo ambalo limelalamikiwa na wananchi walio wengi huku baadhi wakisema ni mambo ya kisiasa.
Akizungumzia tukio hilo jana mjini hapa, Nahodha alisema tukio hilo limemsikitisha yeye na Serikali yake kwa wananchi kuamua kuchukua sheria mkononi na kusababisha athari kubwa.
Alisema kitendo hicho ni cha kiuhalifu na kimevunja sheria za nchi hivyo kama mwenye dhamana ya kusimamia mambo ya ulinzi na usalama hawezi kuvumilia tukio hilo. Amesema tayari hatua za kuwasaka waliohusika zimeanza na baadhi yao wanashikiliwa na Polisi.
Akifafanua zaidi kuhusu tukio hilo,Nahodha alisema tangu mabanda hayo yalipochomwa kumekuwepo na taarifa nyingi ambazo zinaelezea sababu za tukio hilo.
“Kazi yetu kama wizara tunachokifanya ni kuhakikisha wote ambao wamehusika na tukio hilo wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.Kazi yetu Serikali ni kuhakikisha wanaovunja sheria wanachukuliwa hatua,”alisema.
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya nchi hakuna aliye juu ya sheria hivyo kwa aliyehusika akibainika na Mahakama ikathibitisha kuwa amehusika kuchoma vibanda hivyo hataachwa na kuongeza sheria lazima ichukue mkondo wake.
Kuhusu taarifa kuwa waliochomewa mabanda hayo ni wafanyabiashara kutoka Tanzania Bara,Nohodha alijibu kuwa yeye ni Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo si suala ni wananchi kutoka upande gani hilo halina mantiki kwake bali anachoaangalia ni usalama wa Watanzania wote.
Alisisitiza kuwa “Mimi kama Waziri wa Mambo ya Ndani nimepewa jukumu la kusimamia ulinzi nausalama, wa maisha ya raia na mali zao kwa nasema kitendo hicho ni uvunjifu, uhalifu na jinai kwa kuwa kuna mali zemochomwa.”
Kuhusu kulipwa fidia kwa waliochomewa mabanda yao alisema Wizara yake haina jukumu la kulipa fidia bali jukumu lake ni kuhakikisha sheria zilizopo zinafuatwa.
Alisema Sheria inapovunjwa taratibu zilizopo kisheria zinafuatwa ili yule aliyevunja sheria hiyo apelekwe mahakamani ili iweze kutoa maamuzi.