Mzee Kingunge Ngombare Mwiru
Babu yetu mzee Kingunge Ngombare Mwiru amenukuliwa kwenye vyombo vya habari Leo akipinga hoja ya Tanzania kuruhusu raia wake kuwa na Uraia Pacha (Dual Citizenship). Namshukuru mzee Kingunge kwa kujitokeza hadharani na kupinga, maana ni vizuri tukawajua wazi wale wanaopinga na wale wanaounga mkono hoja hii muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu. Vita vya kuviziana au vya chini kwa chini huwa vina madhara makubwa sana, ndio maana pia nampongeza waziri wa mambo ya nje, Mh. Bernard Membe kwa kujitokeza na kuitetea hoja hii mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba hivi karibuni. Kitu ambacho nahisi ndio kimemshinikiza mzee Kingunge nae kujitokeza na kueleza dukuduku lake. Nasema haya yote ni muhimu wakati tunajadili hoja hii.
Mzee Kingunge hakufafanua kwa kina anachopinga, ila kwa nukuu niliyoisoma kwenye gazeti la The Gurdian, Kingunge alisema,
“‘The matter of dual citizenship is really disappointing me considering that we were fighting to get nationality from the British and we were not freely given,” he said, expressing surprise at the ruling party’s decision of supporting dual citizenship in the constitution. “I strongly reject this proposal’ ” (The Gurdian, 2013).
Pia, The Gurdian lilimnukuu Kingunge akisema kuwa, “those who propose dual citizenship have their interest because they want that nationality for financial interest”
Cha kusikitisha zaidi, Kingunge alinukuliwa kupinga hoja kwamba uraia pacha utasaidia Watanzania waliopo ughaibuni kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi yao (Tanzania) kupitia uwekezaji kwa kusema kwamba “kuna nchi nyingi zisizoruhusu uraia pacha na bado raia wake wanasaidia nchi zao”(The Gurdian, 2013). Nafikiri mzee wetu Kingunge inabidi afanye uchunguzi wa kina kuhusu suala hili na atambue dunia ilipo na inapoelekea kabla hajaendeleza jitihada za kuturudisha nyuma kwenye hoja ya uraia pacha. Nasema hivyo kwasababu ningependa Mzee Kingunge na Watanzania wenzangu tukumbuke masuala kadhaa yafuatayo.
Karibia kila mtu anashuhudia jinsi dunia sasa inavyokuwa kijiji komoja, ambapo kila nchi sasa inabidi iwe na mikakati maalum ya kukaribisha na kukabili mabadilko haya. ukuaji wa teknolojia kama ya intaneti na vifaa vyepesi vya mawasiliano (mobile devices), ukichanganya na urahisi wa uhamaji wa watu katika kila pembe za dunia hii, kunatimiza ndoto za watu wengi haraka zaidi kuliko ilivyodhaniwa.
Nchi yingi zikikabiliwa na mitihani hii ya maendeleo haya ya kidunia, zimeamua kujidhatiti kwa kutumia rasilimali zake za utamaduni na watu, ili kukabiliana kikamilifu na mabadiliko haya ya kidunia. Kukubali na kuhalalisha Uraia pacha ni moja ya njia, ambayo nchi nyingi zimeamua kutumia, ili kuhakikisha zinaendelea kunufaika na michango ya raia wake, ambao wapo sehemu mbalimbali duniani kutokana na sababu nyingi, zikiwemo fursa za elimu, ajira, na usalama. Raia hao wamelazimika kuendelea kuishi nje ya nchi zao, bila kupoteza mapenzi kwa nchi zao za asili na siku zote wameendelea kutambulika kama Watanzania, wakenya, waganda, wanaijeria, na kadhalika….kwanza, kabla ya kuitwa Wamarekani, Waingereza au Wajerumani.
Kwa mfano, kama walivyo “African American” (kutambua asili yao ya Uafrika) wapo pia “Tanzanian American”, Kenyan American, Nigerian American, na kadhalika. Waliitwa “African American” kwasababu ukisoma historia ya Marekani utagundua kwamba vizazi vilivyofuata baada ya watumwa halisia kufa, hawakujua haswa wametoka nchi gani Afrika. Ndio maana vizazi vya watumwa hawa leo hii wameanzisha kampeni maalum ya kujua kule watokako. kampeni hizi kwa marekani zinaongozwa na mwanahistoria mahiri, Dr. Henry Luis Gates kupitia vipindi vyake maalum vya runinga “PBS African American Lives” (finding your roots).
Wengi wa Waafrika hawa huwa wanatoa machozi pindi wanapofahamishwa kwamba huenda(sio hata asilimia 100) wakawa wanatokea nchi fulani na wengine uamua kufunga safari na kuitembelea nchi husika. Sasa ndugu zangu inasikitisha sana kumsikia mzee Kingunge akisema “The issue of dual citizenship will completely take out the patriotism as each country has its own policies toward patriotism ” (The Gurdian, 2013). Hili sio suala la kuchukulia kiurahisirahisi na kutumia hoja ya “uzalendo” (patriotism) kwamba ni kigezo cha kumzuia mtu asiwe a pasi mbili, Je kwa kuzingatia yale machungu yanayowakumba wamarekani weusi sasa, tunafikiri kwamba asili ya mtu, mapenzi na uzalendo vitatoweka kwa kuwa tu eti mtu anakaratasi ya nchi nyingine?
Baadhi ya nchi zimeshabadilisha sheria zao baada ya kazingatia kwa kina mabadiliko ya dunia, na baadhi zimeweka masharti maalum katika sheria zao za uraia pacha, ili kulinda maslahi ya nchi. kwa mfano, kuanzia mwaka 2004, raia wa South Afrika wanaweza wakawa na pasi ya nchi nyingine, ukizingatia kwamba wametimiza miaka 18 na wameomba suksa maalum kabla ya kuchukua pasi ya nchi nyingine. Na waustralia na wa New Zeland hawajali una pasi ngapi, almuradi umetimiza masharti ya kuwa raia wao kwa vigezo vya kuzaliwa(by birth) au vya kuomba(by naturalization). Kwahiyo, hii inaonyesha kwamba jibu hapa sio kukataa hoja moja kwa moja kwamba haifai kama anavyodai Mzee Kingunge, bali tuangalie mifano ya wenzetu waliokwisha fanya wamefanya vipi na wanaendelea kunufaika vipi.
Itakuwa ni kosa kubwa kama nitaendelea kuzitaja nchi hizi, bila kuitaja nchi ya Kenya, ambayo ni jirani yetu wa karibu na tunashahabiana na kushirikiana katika masuala mengi tu. Wakenya waliliangalia suala hili kwa kina wakati wa mchakato wa mabadiliko ya katiba yao hivi karibuni, na hatimaye kukubaliana kwamba linafaa kwa maendeleo ya nchi yao, na hivyo kuliweka kwenye katiba.
Wakati Wakenya wanapambana kuhusu suala la uraia pacha, walizingatia faida kadhaa (zipo nyingi), ambazo Kenya ingezipata. Faida hizi ndio faida, ambazo Tanzania pia itazipata endapo tutakuwa makini katika suala hili. Ningependa kuzitaja baadhi ya faida hizo kama ifuatavyo:
Kwanza, Watanzania ambao wana uraia wa nchi nyingine, kwasasa wanalazimika kuomba viza ya ugeni (visitor’s visa) kuingia Tanzania na pia kuomba ruksa ya kukaa na kufanya kazi Tanzania kama wanataka kufanya hivyo. Uraia pacha, utaboresha suala hili, na kurahisisha mizunguko baina ya Tanzania na nchi husika (nchi ya pasi ya pili ya Mtanzania) na kuongeza chachu ya uwekezaji wa Watanzania katika nchi yao ya asili. Kujibu hoja ya mzee wetu Kingunge katika suala hili la uwekezaji, ni kwamba kwasasa watanzania na waafrika wengine, ambao nchi zao haziruhusu uraia pacha, wanawekeza sana (ikiwemo kutuma pesa za misaada mbalimbali), lakini katika mazingira magumu kutokana na kwamba michango yao haitambuliki kisheria.
Pia, kwa ufafanuzi zaidi, tofauti ya muwekezaji mzalendo(Mtanzania mwenye pasi mbili) na muwekezaji mgeni, ni kwamba Wawekezaji wageni mara nyingi huwa na hofu sana ya kuwekeza kwenye nchi za “Dunia ya Tatu”, lakini Mtanzania asili hana hofu hiyo (labda nyakati za vita) kutokana na mahusiano yake ya kiudugu (kinship) na ufahamu wa utamaduni wa uendeshaji wa mambo nchini mwake, hivyo basi kuwa rahisi kwake kujitosa bila hofu kwenye fursa za kibiashara.
Pili, Watanzania asili, ambao wanaishi ughaibuni wataendelea kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii nchini Tanzania kutokana na uzoefu wao wa kipekee wanaoupata kwa kuishi kwao kwenye nchi hizi zilizoendelea, hivyo basi ni muhimu kutengeneza mazingira mazuri kwa wao kuendelea kushiriki na kunufaisha nchi. Hapa nazungumzia pia wale wasomi wengi ambao wameloea ughaibuni kutokana na sababu ambazo nimezitaja hapo awali.
Hili sio suala geni, ndio maana tunaona hata hizi nchi kubwa kama Marekani, Ujerumani na Wingereza wanautaratibu maalum wa kukaribisha wageni, na baada ya muda kuwapa uraia, ili wachangie maendeleo zaidi kwa kutumia elimu zao na uzoefu waliokuwa nao kutoka kwenye nchi zao. “USA Diversity visa program” maaarufu kama “Green Card” ni maalum kwa kufanikisha hili na hata Wamarekani na nchi nyingine kubwa hawana ugomvi na suala la uraia pacha (wengi wakishatoa uraia, hawamlazimishi mtu kuukana uraia wa nchi yake ya asili), ili mradi mtu havunji sheria za nchi zao kwa kigezo cha uraia wake wa nchi nyingine.
Sasa kama nchi kubwa zinatumia fursa hii, iweje sisi leo kuwekeana masharti magumu, wakati bado tupo katika mapambano ya kuiendeleza nchi yetu? Tuna hitaji Kila kichwa kishiriki popote kilipo wakati wowote ule. Vinginevyo, wale maadui watatu aliotutajia Baba wa taifa miaka takribani 40 iliyopita, yaani, Ujinga, Maradhi, na Umasikini vitaendelea kututesa.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.
Naomba kuwasilisha,
Hashim Rungwe Jr.
www.thehabari.com
Info@thehabari.com
1/9/2013