Mzee Auwawa Kikatili Wilayani Rombo

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz


MKAZI wa Kijiji cha Mahida Nguduni, Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro, Dominick Kavishe (65) mkulima ameuwa kikatili kwa kuchomwa na vitu vyenye ncha kali katika sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wasiofahamika. Akizungumzia tukio hilo kwa njia ya simu na mtandao huu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa kwa sasa hawezi kuzungumza lolote juu ya tukio hilo kwani yupo nje ya ofisi.

Mmoja wa viongozi wa Kijiji cha Mahida Nguduni ambaye hakutaka kutajwa jina lake alisema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana majira ya saa tatu usiku. Mke wa Marehemu, Meristela Kavishe alisema yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kugundua kifo cha mumewe kwani kabla ya tukio hilo alikuwa amemsindikiza jirani yake aliyemtaja kwa jina la Taudensia Kiwela na aliporudi hakumkuta mumewe hivyo kuanza kumtafuta. Alisema baada ya kuzunguka nyuma ya nyumba yao ndipo aliukuta mwili wa marehemu ukiwa unatokwa na damu nyingi huku ukionekana kuchomwa sehemu mbalimbali za mwili na kitu chenye ncha kali.

Mchungaji wa Kanisa la TAG, Leopard Kauki ambaye ni jirani wa marehemu alisema kuwa alisikia kelele usiku akiwa nyumbani kwake na alipoenda eneo la tukio alikuta jirani yake huyo akiwa ameuawa na hivyo akatoa taarifa kituo cha polisi. Wananchi wa kijiji hicho wamelaani kitendo hicho na kukiita ni tukio la kikatili na kuliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi zaidi ili kufanikisha kuwakamata watu wote waliohusika na tukio hilo.