Na Mwandishi Wetu,
MWALIMU Mkuu wa Shule ya Msingi Makumbusho, Mwalimu Lyimo leo ameamua kuwapa ukweli wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule hiyo, baada ya kuwapa ukweli juu ya malezi ya watoto katika kikao alichoitisha kujadili maendeleo ya wanafunzi shuleni hapo.
Kikao hicho pia kilijadili wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika katika shule hiyo ili kujua namna ya kuwasaidia wanafunzi wa aina hiyo. Kikao hicho ni moja ya mikakati aliyojiwekea mwalimu huyo kuhakikisha shule inakuwa na mikutano ya wazazi na walimu wa madarasa mara kwa mara ili kujadili maendeleo ya mwanafunzi shuleni hapo.
Mama Lyimo katika mazungumzo yake amelaani vikali vitendo vya wazazi kutotoa ushirikiano hasa wanapopewa taarifa kuwa watoto wao hawajui kusoma na kuandika. Kuhusiana na hilo ameahidi mwakani kutopokea mwanafunzi wa darasa la kwanza asiyepitia shule ya awali (chekechea) na atawatimua wale wanafunzi wasiokuwa na maendeleo mazuri na wazazi hawaoneshi ushirikiano.
Katika kikao hicho baadhi ya wazazi walilalamikia walimu kutokuwa makini madarasani na kuwalazimisha watoto wabaki tuisheni, jambo ambalo husababisha watoto wasio na uwezo wa kusoma tuisheni kukosa masomo kamilifu, kwani masomo yote hufundishwa zaidi tuisheni na sio madarasani kama inavyotakiwa.