Na Mwandishi Maalum
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amevitaka vyombo vya habari nchini kusaidia wananchi kwa kutoa habari njema na kuepukana na habari za uchochezi zinazoweza kuitenganisha jamii na kuvuruga amani iliyopo nchini.
Mzee Mwinyi ameyasema hayo April 17, 2013 nyumbani kwake Mikocheni jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari aliouitisha kufafanua kauli aliyoita hivi karibuni kuhusu kuchinja, na kuripotiwa kwa namna ambayo imeleta maana nyingine na kusababisha malumbano.
Rais huyo Mstaafu alisema kwamba Tanzania haina dini bali watu wake ambao ni wamoja ndiyo wenye dini, na kusisitiza kwamba si vyema wananchi wakabaguana kwa imani za kidini jambo ambalo amelitaja ni la hatari kwa mustakabali wa amani katika Taifa.
Kuhusu kauli aliyotoa, Mwinyi alisema: “Si kweli Mzee Ruksa katoa ruksa ya watu kutengana, Sikutoa ruksa hiyo. Hivyo, kama watu wana dharura (katika suala la kuchinja) wavumiliane kama ilivyokuwa toka enzi za ukoloni wa Ujerumani na Uingereza”.
“Nilichokisema ni kwamba kama mtu anachinja kwa matumizi yake na kundi lake asiingiliwe, ila kama ni kwa biashara hapo ni lazima kuwa waangalifu kwa kuzingatia maamrisho ya dini zetu”.
“Ni vyema tukubaliane kwamba kwa miaka mingi toka utawala wa Ujerumani, Uingereza na hivi leo miaka 50 baada ya Uhuru hakukupata kuwa na changamoto kama hii – Kuna nini sasa hadi tukosane?”
“Mimi nitakuwa mtu wa mwisho kuona Waislamu na Wakristo wakitengana maana utakuwa mwanzo na mwisho wa wetu maana tutatengana kwa kila jambo. Huu ni wakati wa kusogeleana”, aliongezea.
Alihimiza kuwepo kwa mazungumzo ya pande zote mbili ili kuendeleza muelewano wa enzi na enzi, na pia aliwaomba wazee wenzie wasaidie katika kuzungumzia kutatua suala hili. “Wazee lazima tulisemee suala hili na nyie wanahabari msaidie kueneza habari njema ambazo zitasaidia kutuliza wananchi”
Aliwataja wanaochochea suala la kuchinja kuwa ni watu watundu ambao wanatakiwa kuelimishwa kwamba wanachokifanya si jambo jema na linahatarisha amani na utulivu wa taifa letu
“Mtengano huo hautoishia hapo kwenye kuchinja. Na kwa nini tutengane?” alisema.