Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi {CCM} na Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete yuko nchini China kwa ziara ya kikazi ya siku sita (6) iliyoanza Aprili 17 mpaka April 23, 2016.
Ziara hiyo ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi inafuatia mualiko rasmi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Kikomunisti cha China (CCP) na Rais wa China Mheshimiwa Xi Jinping.
Akiwa nchini China, anatarajia kukutana na viongozi wa juu wa Chama Cha CCP na viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na kufanya nao mazungumzo yanayolenga kuimarisha uhusiano kati ya CCM na CCP na serikali za nchi hizo mbili ulioasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere na Muasisi wa Taifa la China Mwenyekiti Mao Tse Tung.
Mhe Kikwete anatarajia kutembelea Jimbo la Fu Zhou, jimbo ambalo Rais wa sasa wa China amefanya kazi zake za siasa kwa miaka 18, zilizompatia umaarufu na uaminifu kwa watu wa China na kupelekea kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCP na Rais wa China.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa CCM Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ameongozana na wajumbe watatu wa Kamati Kuu Mhe Abdallah Bulembo, Dkt Maua Daftari na Mama Zakhia Meghji. Pia ameongozana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu Dkt Titus Kamani, Mwenyekiti wa Wilaya ya Mkalama Dkt Charles Mgana na maafisa wawili wa Ofisi za Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi.