Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Adam Ng’imba amepokea maombi ya kuhamasisha mchezo wa masumbwi katika halmashahuri hiyo baada ya mchezo huo kuonesha uhai kwa kipindi hiki tofauti na hapo awali.
Maombi hayo yaliyopelekwa na kamati ya kufufua mchezo wa masumbwi Kisarawe ikiongozwa na Bondia Mbaruku Heri, Kocha wa mchezo wa ngumi nchini, Rajabu Mhamila ‘Super D’ pamoja na wadau wengine wa masumbwi nchini wakiwemo Saidi Chaku na Masudi Bakari ambao walipeleka barua kwa ajili ya kurudisha hamasa ya mchezo wa masumbwi.
Akizungumza mara baada ya kusoma maombi hayo Ng’imba alisema amepokea kwa moyo mmoja maombi hayo na sasa watahamasisha mchezo huo na ngumi kupigwa kama zamani. “…Nakumbuka mabondia wengi akiwemo Habibu Kinyogoli ‘Masta’ ametokea huku huku Kisarawe na mkumbuke kuwa bondia wa ngumi za ridhaa anaetamba kwa sasa na aliyetuwakilisha katika mashindano ya Olimpic yaliyomalizika hivi karibuni Selemani Kidunda naye anatoka katika Wilaya ya Kisarawe hivyo tunaweza kuhakikisha ngumi zinarudia enzi zake,” alisema kiongozi huyo.
“…Naomba niwaahidi kuwa ngumi hizi zitapigwa katika viwanja vya wazi ili kila mtu ashudie mchezo wa ngumi unavyorudi upya katika wilaya hii, naomba wapenzi mashabiki wa mchezo wa masumbwi wakae mkao wa kula siku ya Aprili 26 ngumi zitapigwa katika uwanja wa bomani ili kila mtu ajionee mwenyewe,” alisema.
Aliongeza kuwa ataendelea kutafuta wafadhili ili walete hamasa ya mchezo wa ngumi katika wilaya hiyo ambayo imejinyakulia umaarufu mkubwa mpaka sasa kupitia mchezo wa ngumi..nita hakikisha tunanunua vifaa vya mchezo ili vijana wapate kuendelea kushiriki mazoezi na atimae waje kurudia enzi za Kinyogoli,” alisisitiza.
Naye Mkuu wa msafara wa kuhamasisha mchezo wa ngumi katika wilaya hiyo, Mbaruku Heri alisema atahakikisha siku hiyo analeta vijana wengi wakali wanaotamba katika mchezo huo wa masumbwi kwa sasa kama vile Ibrahimu Class ‘King Class Mawe’, Hamza Mchanjo, Thobias Adaut, Husein Pendeza, Said Uwezo, Adamu Ngange, Ambokile Chusa, George Dimoso, Twalibu Mchanjo na wengine wengi wanaofanya vizuri katika masumbwi kwa sasa.