Na Janeth Mushi, Arusha
MWENYEKITI wa Kata ya Lemara iliyopo katika Manispaa ya Arusha, George Madumba (54) amekutwa amekufa katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Rockies iliyopo eneo la Tengeru Wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi, Leonard Paul alisema kifo hicho kilitokea juzi saa 9:00 alasiri katika nyumba hiyo na kuongeza kuwa awali Madumba aliingia kwenye nyumba hiyo saa 4:00 asubuhi.
Kaimu huyo alisema kuwa Madumba aliingia katika nyumba hiyo akiwa na mwanamke asiyefahamika na ilipofika saa 8:00 mchana mwanamke huyo alitoweka. Paul alisema baada ya muda mhudumu wa nyumba hiyo, Blandina Michael (30) mkazi wa Tengeru aliingia chumbani humo kwa lengo ya kufanya usafi ndipo alipogundua Madumba amefariki.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Maount Meru. Awali mmoja wa mwanafamilia ya marehemu huyo alidai kuwa marehemu siku ya tukio alienda kanisani na alipotoka alidai kuwa anakwenda Tengeru wka ajili ya kununua malisho kwa ajili ya ng’ombe, ambapo muda ulipozidi kwenda hadi majira ya jioni wanafamilia walianza kupigiwa simu na polisi kupitia simu ya maerehemu huyo na kuwapa taarifa kuwa amefariki dunia.
Wakati huo huo, Nyumba ya Familia inayomilikiwa na familia ya Mzee Kito yenye vyumba vitatu na wapangaji wawil imeteketea kwa moto na kuisha kabisa. Kaimu Paul alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 6:00 mchana Kitongoji cha Maji ya Chai Tarafa ya King’ori wilayani Arumeru na kuongeza kuwa nyumba hiyo iliyokuwa na wapangaji wawili ambao ni Anna Jackson (48) na Rose Sadick (58) iliungua vitu vyote na chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.