Na Joachim Mushi
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP, Said Mwema amesema Watanzania wasiwe na hofu juu ya kuendelea kwa vitendo vya kigaidi katika nchi ya jirani ya Kenya, kwani Jeshi la Polisi Tanzania tayari limejipanga vyema kukabiliana na vitendo hivyo.
IGP Mwema ametoa taarifa hizo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusiana na masuala mbalimbali yakiwemo ,atishio ya ugaidi yaliyoanza kujitokeza katika nchi ya jirani ya Kenya, Uharamia unaojitokeza katika ukanda wa Bahari ya Hindi na matukio mengine yanayojitokeza yakiwemo ya ajali za barabarani.
“Jeshi la Polisi linapenda kuwaondoa wasiwasi wananchi juu ya Ugaidi unaoendelea katika nchi ya jirani ya Kenya, kwamba, tayari tumejipanga vyema kwa kuimarisha ulinzi na hasa maeneo yote ya mipakani na kazi hii inafanyika kwa ushirikiano na vyombo vingine vyote vya ulinzi na usalama,” alisema Mwema katika taarifa yake.
Akifafanua zaidi alisema kuna matukio ya uharamia na uhamiaji haramu ambayo yamekuwa yakijitokeza katika ukanda wa Bahari ya Hindi hususani katika mikoa ya Pwani, Mtwara na Lindi na hivyo katika kipindi cha mwaka huu maharamia wapatao 13 wamekamatwa na tayari wamefikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Hata hivyo amewataka raia kuchukua tahadhali ya watu ama makundi ya watu watakaowatilia mashaka kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa ili hatua za haraka za kiusalama ziweze kuchukuliwa.
“Wanapoona kitu ambacho si cha kawaida watoe taarifa kwa kutumia namba za simu zifuatazo 0787 668306, 0222138177, 111, 112 na namba za Makamanda wa mikoa, wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCDs) na RTOs zilizokwishasambazwa hadi ndani ya mabasi,” alisema Mwema.