WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesema suala la uwekezaji hapa nchini haliwalengi watu wa nje tu bali hata wa ndani wanaweza kuwekeza hata kama ni kwa kiwango kidogo.
Ametoa kauli hiyo jana usiku, wakati akizungumza na wakazi wa mikoa ya Rukwa, Ruvuma na mkoa tarajiwa wa Katavi katika chakula cha jioni ambacho aliwaandalia kwenye makazi ya Waziri Mkuu, Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Wakazi hao zaidi ya 100 walikuwa wamealikwa kuja jijini Dar es Salaam kushiriki tamasha la Utamaduni la mikoa ya Rukwa na mkoa tarajiwa wa Katavi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara. Tamasha hilo lilifanyika Novemba 25-27, 2011, katika kijiji cha Makumbusho jiini Dar es Salaam.
Akifafanua kuhusu uwekezaji Waziri Mkuu alisema yeye alipochukua mkopo waliopatiwa wabunge wa sh. milioni 90, hakuona haja ya kununua gari bali aliamua kuwekeza katika ujenzi wa nyumba ya kulala wageni kijijini kwao, Kibaoni wilayani Mpanda.
“Nilichukua mkopo mwingine benki ya NMB na kuamua kujenga vyumba 24 pale kijijini kwetu. Kama ningetaka ningechukua mafundi wazuri kutoka Kariakoo, (Dar es Salaam) lakini niliamua kutumia mafundi wa kijijini ili kutokana na zile fedha nao pia waweze kununua bati na kuezeka katika nyumba zao, jambo ambalo limewezekana,” alisema.
“Ujenzi wa vyumba 24 karibu unakamilika, … kiasi kingine cha fedha nililima shamba la mahindi na nikafanikiwa kuvuna magunia 380,” aliongeza.
Waziri Mkuu anasema aliamua kuuza magunia 300 kati ya hayo aliyovuna na kupata sh. milioni 11 ambazo aliziwekeza tena katika mradi wa ufugaji nyuki kijijini kwao na Dodoma.
“Nina mizinga 250 kule Dodoma na Kibaoni (kijijini kwao) nina mizinga 600, kila mzinga unauzwa sh. 50,000/- na kila mmoja una uwezo wa kutoa lita 10 za asali. Bei ya asali hapa mjini ni sh. 10,000/- kwa hiyo katika kila mzinga unaweza kupata sh. 100,000/-,” alisema.
Alisema suala la uwekezaji ni muhimu na haliepukiki na kumtaja Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi ambaye alikuwepo katika hafla hiyo kwamba ni miongoni mwa wawekezaji wadogo kwani ana ekari 200 za mahindi na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Kanali Antonio Mzurikwao kuwa naye ana ekari 100 za mahindi. “Hawa nao ni wawekezaji lakini tunawaita wawekezaji wadogo,” alisema.
Akifafanua kuhusu uwekezaji, Waziri Mkuu alisema nchi zote zilizoendelea zilifaulu kufiki hatua hiyo kwa kupunguza idadi ya wakulima wadogo na kuongeza idadi wa wakulima wakubwa. “Mkiona wakulima wadogo ni wengi mjue kuwa bado hamjapunguza umaskini,” aliongeza.
Alisema Taifa bado linakabiliwa na changamoto ya kupunguza umaskini kwa kuhahakikisha kwamba kuna uzalishaji wa chakula cha kutosha ili watu kwanza washibe lakini pia akaongeza kusema kwamba inabidi uzalishaji uwe na tija ili wakulima wapate mazao mengi na kujiongezea kipato.
Akitoa shukrani katika hafla hiyo, Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi aliwashukuru wajumbe wa Kamati za maandalizi katika mikoa ya Dar es Salaam na Rukwa kwa maandalizi mazuri hadi wakafanikisha tamasha la utamaduni wa mikoa hiyo miwili.
Alisema utamaduni na lugha ni vitu vikubwa vinavyotambulisha utaifa wa watu na kwamba bila utamaduni hakuna Taifa. “Taifa lisilo na utamaduni ni Taifa lililokufa… tujihadhari kwani kumbukumbu zetu nyingi zimeanza kutoweka… wazo la kuanzisha hifadhi ya kumbukumbu kule nyumbani ni jema sana nami nitakuwa tayari kuwaunga mkono wakati wowote,” alisema huku akishangiliwa.
Aliwataka wana-Rukwa na mkoa tarajiwa wa Katavi wawe na umoja na kusisitiza kwamba siku zote wawe na mwamko mmoja wa kuleta maendeleo katika mikoa yao ya Rukwa na Katavi. “Tutumieni kila inapowekezekana sisi ambao tuko katika nafasi za uongozi ili tusaidie kuleta maendeleo kwa mikoa yetu,” alisema.