KAMPUNI ya kuzalisha umeme nchini Marekani, ‘Symbion Power’ inafanya mazungumzo ya mwisho kuinunua mitambo ya Dowans ambayo sasa kwa muda imekuwa haifanyi kazi kwa muda sasa tangu izimwe kwa mara ya mwisho.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na baadhi ya wawekezaji jijini Dar es Salaam mazungumzo yanafanywa kwa muda sasa Dar es Salaam kati ya mmiliki wa mitambo wa Dowans na kampuni ya Symbion ili kuweza kufikia muafaka na mitambo kununuliwa na kampuni hiyo.
Taarifa zinaeleza kuwa mazungumzo ya ununuzi wa mitambo hiyo yanayoendelea kati ya pande huenda yakamazilizika mwishoni mwa juma hili kwani tayari maafikiano ya awali yamefikiwa na pande zote.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Symbion, Paul Hinks juzi alilithibitishia gazeti moja la kila siku nchini linaloandika kwa lugha ya Kiingereza kuwa ni kweli wamekuwa wakifanya mazungumzo na kampuni ya Dowans kwa ajili ya kununua mitambo hiyo.
“Ndio ulichokisikia ni kweli…upo sahihi tunafanya mazungumzo,” alisema Hinks alipokuwa akifanya mazungumzo na gazeti hilo la Kiingereza juu ya kinachoendelea.
Mkurugenzi huyo alisema nia yao ni kuinunua na kuimiliki kwa asilimia 100 kama mali ya Symbion na si kwa kumiliki kwa kuchangia hiza kama ilivyo kwa mitambo mingine. “Tunataka kuwa wamiliki wa mtambo wote bila kuchangia na yeyote…tunataka umiliki wetu uwe wa asilimia 100,” alisema Hinks.
Symbion ambayo ni miongoni mwa kampuni kubwa wazaziliza wa nishati ya umeme katika maeneo kadhaa ulimwenguni, wamethibitisha kuwa mazunguzo ya kuinunua Dowans yanaweza kukamilika ndani ya wiki hii.
Akifafanua zaidi Hinks alisema kununuliwa kwa mitambo ya Dowans na kampuni yake itakuwa ni hauweni kubwa kwa Watanzania wengi ambao sasa hivi tayari wapo kwenye mgawo mkubwa wa umeme, unaoathiri shughuli anuai za viwanda na matumizi ya kawaida maeneo tofauti.
“Nasema itakuwa hauweni kwa Watanzania kwa kuwa mara baada ya kumalizika kwa mchakato wa manunuzi mara moja tutawasiliana na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (TANESCO) na kuwasha mitambo ianze kufanya kazi mara moja,” alisema Hinks.
Aliongeza kuwa isinge kuwa raisi wao kufanya mazungumzo na TANESCO au Serikali juu ya namna ya kuwashwa kwa mitambo hiyo, ilhali bado hawajamalizana na wamiliki katika mazungumzo yanayoendelea ya kuinunua.
“Tutakuwa katika sehemu nzuri ya kufanya mazungumzo na TANESCO au Serikali juu ya kuwashwa kwa mitambo baada ya kumaliza mazungumzo haya. Hii itakuwa hatua ya pili baada ya ile ya kwanza (mazungumzo na Dowans),” alisema Mkurugenzi huyo Mtendaji.
Hata hivyo alipinga kutoa taarifa zaidi ikiwemo bei ambayo wanataka kuinunulia mitambo hiyo na kudai vyote hivyo vitatolewa kwa vyombo vya habari baada ya mchakato mzima kukamilika.
Aliongeza kuwa mazungumzo yanayoendelea kati yao na kampuni ya Dowans hayaathiri kisheria kwa namna yeyote juu ya mvutano uliopo (kimalipo) kati ya TANESCO na Dowans.
Alisema mazungumzo hayo hayawaathiri wao kama wanunuzi wa mitambo hiyo kwa kuwa wanachokizungumzia ni juu ya kununua mitambo lakini si malipo ambayo Dowans imekuwa ikivutana na TANESCO kisheria.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema mazungumzo ambayo yanaendelea kati ya Dowans na kampuni ya Symbion juu ya ununuzi wa mitambo hiyo yatawanusuru Watanzania takriban milioni 44 ambao kwa sasa wapo katika mgawo mkubwa wa umeme kufuatia ratiba ya mgawo wa saa 12 iliyotolewa na TANESCO hivi karibuni.