Mweka Hazina Wilaya ya Monduli atuhumiwa kwa ‘ufisadi’

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye

Na Mwandishi Wetu, Arusha

JESHI la Polisi mkoani hapa linamshikilia Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Julius Masheri pamoja na Mkuu wa Usafirishaji (TO), Bakari Jabu kwa tuhuma za kughushi matumizi hewa ya mafuta.

Kwa mujibu wa chazo chetu cha habari kinaeleza kuwa wanaohojiwa katika tuhuma hizo ni pamoja na wafanyakazi wa Benki ya NMB Tawi la Monduli na kampuni binafsi inayouza na kusambaza mafuta mkoani Arusha, ambayo pia iliwahi kuhusishwa na
kashfa ya malipo ya Fedha za EPA.

Taarifa zinadai watendaji hao wanatuhumiwa kughushi hundi ya malipo ya lita 2,000 za mafuta aina ya dizeli ya thamani ya sh. milioni 4.2 kwa matumizi ya halmashauri hiyo fedha ambazo inadaiwa zilishalipwa. Mweka Hazina huyo anadaiwa kughushi hati nyingine ya malipo (LPO) ya thamani ya fedha milioni 4.2, na kuiwasilisha Benki ya NMB kwa malipo ya mafuta lita 400 ambayo ilisha lipwa kitambo.

Inadaiwa kuwa baada ya Mweka Hazina kusimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo alikwenda NMB na kushawishi malipo yafanyike kwa njia ya
kuhamisha fedha kutoka akaunti ya halmashauri kwenda akaunti ya kampuni ya mafuta.

Inadaiwa malipo hayo yalifanyika kwa njia hiyo ya wizi kutokana na mweka hazina kuwa nje ya ofisi hali iliyomsababisha kushindwa kupata vitabu vya hundi ili kuandikia malipo hayo na badala yake kughushi sahihi ya mhasibu anayekaimu nafasi hiyo katika hati hiyo ya madai (LPO).

Aidha kitendo hicho kilibainika kufuatia mhasibu huyo anayekaimu nafasi hiyo kutoa taarifa baada ya kuona sahihi yake imeghishiwa katika hati ya madai iliyowasilishwa na Benki ya NMB kwa ajili ya malipo.

Kwa mujibu wa upekuzi uliofanywa wakati huu ambapo mtuhumiwa yuko nje, Mhasibu wake, Emanuel Nabuli amekutwa na kitabu kimoja chenye thamani ya sh. milioni 2.6. Uchunguzi umebaini pia kupotea kwa vitabu viwili vyenye thamani ya sh. 600,000 na kingine milioni 3, ambavyo inadaiwa viliibwa na Mtendaji wa Kijiji cha Moita na kingine Mtendaji wa Kata ya Moita, ambao tayari wamehojiwa na polisi kwa wizi.

Mbali na wakuu hao wa idara kushikiliwa kwa mahojiano, wapo viongozi wa benki ya NMB, wafanyakazi pamoja na mhasibu wa halmashauri hiyo ambao kwa pamoja wanatakiwa kutoa maelezo juu ya tuhuma hizo kabla ya kufikishwa mahakamani.

Aidha inaelezwa kuwa baadhi ya watuhumiwa wamekuwa wakitumia rasilimali za
halmashauri hizo kwa manufaa yao ikiwemo matumizi ya tingatinga linalotumika kuchimba visima wilayani Longido bila taarifa za Mkurugenzi na kisha fedha zilizopatikana kudaiwa kutoweka.

“Mwaka huu mkuu huyo wa usafirishaji aliamuru tingatinga la halmashauri bila idhini ya mkurugenzi liende wilayani Longido kuchimba visima kikiwemo cha Mbunge wa Jimbo hilo, Lekule Laiser ambapo fedha zilizopatikana hazijulikani alipozipeleka,” kilieleza chanzo chetu.

Hata hivyo mtandao huu ulipowasiliana na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa juu ya kushikiliwa kwa watuhumiwa hao alikiri na kudai bado wanawahoji wahusika. Amesema kazi hiyo inafanywa na kikosi cha upelelezi Kituo cha Polisi Kati jijini Arusha. Akili amesema kwa sasa wafanyakazi wawili wa benki ya NMB wanahojiwa na polisi kuhusiana na tuhuma hizo.