Mwanza na Temeke kuvaana nusu fainali Copa Coca-Cola 2012

Copa Coca Cola 2012

*Maxinsure yaipa Twiga Stars vifaa vya mazoezi

Na Mwandishi Wetu

TIMU za Temeke na Mwanza zinapambana kesho Julai 13 mwaka huu katika nusu fainali ya kwanza ya michuano ya Copa Coca-Cola 2012 itakayochezwa saa 2.30 asubuhi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Nusu fainali ya pili itaanza saa 9.30 mchana kwenye uwanja huo huo ikizikutanisha timu za Morogoro na Tanga.

Mechi ya kutafuta mshindi wa tatu na fainali ya michuano hiyo zitachezwa Jumapili ya Julai 15 mwaka huu. Mechi ya mshindi wa tatu itaanza saa 5 asubuhi na kufuatiwa na fainali ambayo itafanyika kuanzia saa 9 kamili alasiri.

Mwanza ilipata tiketi ya nusu fainali kwa kuifunga Kinondoni 3-1 huku Temeke ikitinga hatua hiyo kwa ushindi wa mabao 5-3 dhidi ya Mjini Magharibi. Ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Mara ndiyo ulioipa Morogoro tiketi ya nusu fainali wakati Tanga yenyewe iliilaza Dodoma bao 1-0.

Wakati huo huo; Kampuni ya bima ya Maxinsure imetoa vifaa vya mazoezi kwa timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) vyenye thamani ya sh. milioni 1.3.

Vifaa hivyo ambavyo ni jezi, bukta na soksi 20, vizibao (bibs) 20 na mipira miwili vimekabidhiwa leo Julai 12 mwaka huu kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Ofisa Uhusiano wa kampuni hiyo, Amisa Juma.

Akikabidhi vifaa hivyo, Amisa amesema wamefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa jamii lakini vilevile wameamua kuiunga mkono timu hiyo ambayo wanajua haina mdhamini kutokana na vipaji na uwezo ambao umekuwa ukioneshwa na wachezaji wake.

Pia amezitaka kampuni, taasisi, watu binafsi na Serikali kuiunga mkono timu hiyo ili iweze kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali inayotarajia kushiriki.