Mwanga Katika Sekta ya Utamaduni

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Fenella Mukangara (mwenye nguo ya blue) akicheza ngoma ya wanyasa wakati wa  maadhimisho ya Uanuai wa Utamaduni.

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Fenella Mukangara (mwenye nguo ya blue) akicheza ngoma ya wanyasa wakati wa maadhimisho ya Uanuai wa Utamaduni.


Na Mwandishi wetu
‘Utamaduni ni utambulisho wa taifa.’ Kwa umuhimu wake Serikali ya awamu ya Nne imefanya mengi kuhakikisha kwamba taifa letu linaendelea kujitambua na kutambuliwa ulimwenguni.
Serikali Kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeendelea kuenzi na kulinda historia, mila na desturi nzuri za Watanzania na kuzitokomeza mila na desturi mbaya kwa kuelimisha jamii kupitia vyombo vya habari, machapisho, mikutano na mihadhara mbalimbali kuenzi maadili ya Mtanzania.
Tafiti mbalimbali zinazohusu mila na desturi zimefanyika na kuhifadhiwa. Wizara ilifanya utafiti wa Miviga (Jando na Unyago) kwa jamii za Lindi na Mtwara, utafiti wa mila na desturi zinazosababisha wanawake katika mkoa wa Tanga kutoshiriki vizuri kwenye shughuli za maendeleo ya nchi.
Tafiti nyingine ni kuhusu athari za mabadiliko ya mila na desturi kutokana na wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro kuhamia mkoa wa Morogoro, utafiti wa mila na desturi za Wabarabaig, utafiti kuhusu mabadiliko ya mila na desturi kutokana na vijiji kukaa pamoja vijijini katika tarafa ya Kinampanda wilaya ya Iramba.
Katika kuhakikisha kuwa Lugha ya Taifa (Kiswahili) inaenziwa na kuhifadhiwa, Serikali imekuwa ikifanya tafiti za lugha za asili kwa lengo la kupata misamiati ya kukuza na kuendeleza Kiswahili. Hadi sasa tafiti za lugha za asili za mikoa ya Mwanza, Ruvuma na Singida zimeshafanyika.
Aidha, utafiti wa wa majina fiche 1800 ya lugha za asili katika mikoa ya Morogoro, Pwani, Tanga, Lindi, Mtwara na Dar es Salaam ulifanyika. Majina fiche ni majina ya lugha za asili amabayo yanakuwa na maana Fulani. Tafiti hizi zinalenga kuhifadhi na kuendeleza mila na desturi nzuri ii kuzirithishwa kwa vizazi vijavyo.
Serikali ya Awamu ya Nne imesimamia mchakato wa uanzishwaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo makao yake makuu ni Tanzania Zanzibar.
Uongozi huu pia umewezesha uanzishwaji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kwa lengo la kukusanya, kuhifadhi na kutunza kumbukumbu za harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika ikizingatiwa kuwa nchi yetu ilikuwa kiongozi na mstari wa mbele katika ukombozi huo.
Kutokana na usimamizi na miongozo rafiki inayowekwa na Serikali, Sekta ya sanaa nayo imepata mafaniko mengi katika kipindi cha mwaka 2005 – 2015. Matukio makubwa yamejitokeza na yalikuwa chachu ya kukua kwa sekta hiyo.
Mwaka 2013, Serikali ilirasimishwa kazi za Sanaa. Huu ulikuwa ni mwanzo mzuri na moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika Uongozi wa Awamu ya Nne. Serikali imekuwa ikikabiliana na changamoto ya wizi wa kazi za wasanii ambapo kupitia Bodi ya Ukaguzi wa Filamu imerasimisha tasnia ya filamu na muziki na kufanya mazao ya filamu na muziki kuwekewa stempu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kulipiwa kodi.
Hizi ni juhudi za Serikali kulinda kazi za Wasanii na kuhakikisha kwamba Wasanii nchini wanafaidika na jasho la kazi zao pamoja na kuchangia katika pato la Taifa. Taasisi za Serikali zilizokabidhiwa jukumu la kushughulikia urasimishaji wa tasnia za sanaa ya muziki na filamu, zimekuwa zikikagua na kukamata bidhaa zote za muziki na filamu ambazo hazina sifa ya kuuzwa na kusambazwa katika soko la ndani na kupelekwa nje ya nchi.
Sheria ya Ushuru wa Bidhaa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012, na kupitishwa kwa kanuni zake mwaka 2013 inamtaka kila mfanyabiashara wa bidhaa za muziki na filamu kuhakikisha kuwa bidhaa zote za muziki na filamu zinawekewa stempu za Ushuru wa Bidhaa zinazotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kabla ya kusambazwa.
Taasisi za Serikali zinazohusika katika zoezi hili ni Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bodi ya Ukaguzi wa Filamu Tanzania (TFCB), Chama cha Hakimiliki na Hakishirikishi Tanzania (COSOTA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Taasisi hizo kwa pamoja zimekuwa zikitoa elimu kwa wadau wote wanaojihusisha na utengenezaji, uigizaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa zinazohusika na muziki na filamu pia kuhakikisha kuwa wanakamilisha mchakato wote wa uwekaji stempu za Ushuru wa bidhaa kwa kazi zinazoingizwa katika soko la ndani na zinazosafirishwa nje ya nchi.
Kwa mujibu wa sheria wahusika wote wa uzalishaji, uagizaji toka nje ya nchi na usambazaji wa bidhaa hizo wanatakiwa kufika kwa taasisi hizo ili kusajiliwa na kukamilisha utaratibu wa kusajili na kukaguliwa kwa kazi husika kabla hazijapatiwa stempu za Ushuru wa bidhaa kwa ajili ya kubandikwa kwenye kazi husika.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza, Bibi. Joyce Fissoo anasema utaratibu unawataka wale wote wanaokusudia kushughulika na kazi za muziki kuanzia BASATA. Anasema kuwa baada ya hapo hutakiwa kwenda COSOTA ili kupewa vibali kabla ya kwenda TRA ili kununua stempu. Kwa kazi za filamu wahusika wanatakiwa kwenda Bodi ya Ukaguzi wa Filamu kabla hawajapeleka kazi husika COSOTA na baadaye TRA kwa ajili ya ununuzi wa stempu.
Kila kazi, yaani CD, DVD au kanda zinatolewa stempu mbili zenye namba moja katika mtiririko maalum wa namba (serial number). Stempu moja hubandikwa katika kasha na nyingine kwenye CD, DVD au kanda.
Mkurugenzi wa Sera na Utafiti kutoka TRA, Tonedeus Bw. Muganyizi anasema kuwa kazi yoyote ya filamu na muziki inapaswa kuwa na haki miliki kabla ya kusambazwa ili kuiwezesha TRA kutoa stempu kwa kazi hizo. Hata hivyo, anasema kuwa baadhi ya Wafanyabiashara wanaosambaza na kuuza kazi hizo wamekuwa hakikiuka utaratibu huu na kupelekea Serikali kuendesha operesheni ya kusaka kazi za filamu na muziki zisisokuwa na haki miliki na stempu kutoka TRA.
Juhudi zote hizi ni kuhakikisha kuwa tasnia ya sanaa za muziki na filamu inakuwa rasmi na kumnufaisha msanii na Taifa kwa ujumla kuliko hali ilivyokuwa hapo awali ambapo kazi za sanaa zilikuwa zinadurufiwa kiholela.
Mbali na urasimishaji wa tasnia ya filamu na muziki, mwaka 2014 wakati Tanzania ikifanikiwa kuingia katika soko la kimataifa, mafanikio yamejitokeza kwa mwaka huu kwa baadhi ya wasanii kujikuta wakitajwa na hata kushinda katika tuzo za kimataifa.
Ilikuwa ni ndoto ya muda mrefu kwa msanii wa Tanzania kutajwa kushiriki tuzo za BET, lakini kwa mwaka huu imewezekana na Diamond Platnumz amefanikiwa kukanyaga ‘red carpet’. Hakuishia hapo akatajwa kuwania tuzo za MTV MAMA kwa mwaka huu akatajwa tena kuwania MTV EMA tuzo ambazo pia hazijawahi kumhusisha Mtanzania. Baadaye alipendekezwa kuwania tuzo za AFFRIMA, KORA ambazo zote alishinda huku Lady Jaydee naye akishinda tuzo ya AFFRIMA. Baadaye Diamond akawania tuzo za CHOAMVA.
Katika tuzo hizi za Channel ‘O’ Music Video Awards (CHOAMVA) alizoteuliwa kuwania tuzo nne, Diamond alishinda tuzo tatu kupitia vipengere vya Mwanamuziki Bora Anayechipukia, Mwanamuziki Bora Afrika Mashariki na Video Bora ya Mwaka kupitia wimbo wake ‘My Number One’.
Tuzo nyingine ambazo Tanzania imeshiriki ni ‘Kilimanjaro Tanzania Music Awards’ (KTMA), Tuzo za Chaguo la Watazamaji za African Magic (African Magic Viewers Choice Awards) zilizofanyika nchini Nigeria mwaka 2013 ambapo Tanzania ilipata tuzo ya Filamu Bora ya Kiswahili kupitia Filamu ya A Ray of Hope
Ili kusimamia vizuri sekta ya filamu nchini ambayo inatengeneza ajira hasa kwa vijana, Serikali imeendelea kuimarisha Bodi ya Ukaguzi wa Filamu. Moja ya kazi kubwa ya Bodi hii ni kukagua na kuweka madaraja na kutoa vibali vya maonesho ya filamu. Idadi ya filamu zilizokaguliwa mwaka 2002 ilikuwa ni moja lakini mwaka 2006/2007 ilikagua na kuweka madaraja na kutoa vibali kwa kanda za video 59 ikilinganishwa na filamu 1329 mwaka 2015 ambapo ni ongezeko la asilimia 1008.
Kwa lengo la kulinda maadili ya Mtanzania, filamu zisizozingatia maadili zimekuwa zikifanyiwa marekebisho au kupigwa marufuku kuonyeshwa hadharani. Katika kipindi hicho jumla ya filamu 19 zilipigwa marufuku na jumla ya filamu 55 zilifanyiwa marekebisho ya kimaadili na kiuweledi wa tamaduni za Kitanzania.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili Sekta ya Filamu nchini Bibi. Fissoo anasema kuwa ni wimbi la wizi wa kazi za filamu ambao huwafanya Wasanii kutonufaika na jasho la kazi zao ipasavyo pamoja na ukuaji wa kasi wa technolojia unaowezesha usambazaji wa filamu zisizo na maadili.