RAIA wa Marekani Joycelin Tembi Edward (27) aliyekamatwa wilayani Tarime katika vurugu zilizotokana na mauaji ya watu walioingia kwa kuvamia Mgodi wa North Mara Barrick amehukumiwa jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja.
Mmarekani huyo ambaye ni Mwandishi wa Habari wa gazeti la Toronto Canada, alihukumuwa kutumikia kifungo cha mwaka au kulipa faini faini y ash. 50,000 kutokana na kubainika kuwa aliingia nchini na kufanya kazi bila ya kuwa na kibali cha kufanyia kazi.
Joycelin amehukumiwa na mahakama ya hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya ya Tarime kutumikia adhabu hiyo au kulipa faini lakini aliweza kulipia faini hiyo baada ya kukiri kosa lake na hivyo kuamuriwa kuondoka nchini mara moja mara baada ya kukabidhiwa vifaa vyake.
Akisomewa mashitaka Mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Yusto Ruboroga
ilielezwa kuwa na mwendesha mashitaka wa polisi Kasmir Kiria kuwa Joycelin aliingia nchi hapa Mei 22, 2011 huku akiwa hana kibari cha Idara ya Habari na Maelezo kinachomruhusu kufanya kazi za uandishi wa habari na kujihusisha na uchunguzi wa suala la mauaji ya Nyamongo kinyume cha sheria.
Akiongea na gazeti hili mwandishi huyo alisema yeye ni mwandishi wa
kimataifa na alikuwa nchini Uganda kabla ya kuja hapa Tanzania, na kuwa amekuwa akifuatilia masuala ya migogoro mbalimbali katika ukanda wenye madini na kwamba akiwa nchini Uganda baada ya kusikia taarifa mauaji katika mgodi huo alifika nchini kwa ajili ya kupata taarifa.
Awali katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kamanda wa polisi wa Tarime na Rorya, Costantine Massawe alisema kuwa Joyceline alikamatwa akipiga picha za matukio ya vurugu zikiwemo miili ya watu wanne kati ya watano waliouawa wakati kundi la watu zaidi ya 800 walipovamia mgodi huo wa Nyamongo.
Kamanda huyo alidai jeshi lake lilimtilia shaka, baada ya kuona akiongozana na wafuasi wa Chadema kila mahali, na hivyo kuamua kumfuatilia na ndipo walipomkamata Mei 26 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Kamanda Massawe, Joyceline ambaye baada ya kuhojiwa, alidai kuwa yeye ni mwandishi wa habari anayefanya kazi nchini Uganda na Marekani, alipiga picha hizo katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Tarime.
Mbali na picha za maiti hao, Joyceline pia anadaiwa kufika katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime juzi na kupiga picha watuhumiwa wa uchochezi akiwemo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) na watuhumiwa wenzake saba.
Kamanda Massawe alisema Joyceline mwenye hati ya kusafiria ya Marekani iliyoandikishwa Aprili mwaka huu yenye namba 7100566100, ilionyesha kuwa aliingia nchini Mei 1, mwaka huu na baadaye kuondoka kabla ya kurudi tena Mei 22 na kushiriki upigaji wa picha za Vurugu hizo za Tarime.
-Mwanabidii